April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Chanjo ya UVIKO-19 ni salama’

Na Zena Mohamed,Dodoma

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel amesema chanjo ya Uviko-19 inayoendelea kutolewa nchini ni salama hivyo watanzania waache kuogopa mambo ya mitandaoni yanayopotosha.

Dkt.Mollel amesema hayo jijini hapa wakati akifungua mkutano mkuu wa wadau wa huduma za elimu ya afya kwa umma uliofanyika jijini hapa.

“Tanzania ni Taifa la Mungu, hivyo hatma yake iko mikononi kwa Mungu mnatakiwa mchape kazi na nyinyi waandishi mzingatie maudhui yanayofaa kwenye vyombo vya habari.

“Msiogope yanayoendelea mitandaoni na kwenye vyombo vya habari ni kawaida tu, mambo yatakaa vizuri. Mkachape kazi hayo mengine mtuachie sisi Maronado wenu wao watakuja na wataondoka wakiwa wamefunga goli 0, hali ya chanjo inaenda vizuri,tunaweza kuwaacha wapumbavu na wajinga tukaenda nao,”amesema.

Akizungumzia utoaji wa elimu kwa umma, Dkt.Mollel amewataka wadau hao kuwashirikisha watu maarufu, wasanii na viongozi wa dini ili kufikisha elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa chanjo ya Uviko-19 hasa katika sehemu za vijijini.

Pia amewataka wadau kutokujielekeza katika kufanya semina na makongamano na badala yake bajeti iliyowekwa itumike kuwawezesha wadau kuwafikia wananchi ili kutoa elimu ya afya kwa umma na chanjo ya Uviko 19.

Naye Msemaji wa Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia, Prisca Ulomi akitoa salamu kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo amesema wizara hiyo itashirikiana vizuri na wadau na makampuni ya simu kutoa elimu ya afya kwa umma kwa njia ya Tehama.

“Tanzania sasa ina takribani watumiaji wa mitandao ya kijamii 16.5 milioni na imesambaa kwa asilimia 94 ya jografia kimawasiliano, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutumia teknolojia katika kuwafikia wananchi,”amesema.