May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkulima Steven Mlimbila akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani)hivi karibuni ,mkoani Njombe,

Zao la Parachichi lilivyomnyanyua,Mlimbila kiuchumi

Na David John,TimesMajira,Online

SERIKALI ya awamu ya tano inayongozwa na Dkt. John Magufuli wakati wote imekuwa mstari wa mbele kusisitiza watanzania kujenga nidhamu ya kujiajiri kwani huko ndiko kwenye asali na maziwa.

Viongozi mbalimbali akiwamo Rais Magufuli mara nyingi akiwa kwenye majukwaa kuhutubia amekuwa akisisitiza dhana ya watanzania kuacha kutegemea ajira kutoka Serikalini badala yake kujikita katika sekta binafsi .

Anasema katika serikali anayoiongoza kiu yake kubwa ni kuona vijana na watanzania kwa ujumla wanapata mafanikio ili mwisho wa siku nchi inakuwa sio tegemezi kwa maana kutegemea wahisani ili kuweza kujiendesha.

Katika kuitikia wito huo kijana Steven Mlimbila ambaye ni mkulima wa zao la parachichi kutoka mkoani Njombe Kijijini cha Maheve kilichopo kata ya ramadhani amesema kuwa yeye aliaza kilimo miaka kumi iliyopita huku akijishughulisha na biashara ya kuuza miche ya maparachichi.

Mlimbila ambaye pia ni kijana Mwenye familia ya watoto watatu na mke mmoja amesema kuwa baada ya kujikita katika kilimo cha parachichi ameweza kupata mafanikio makubwa ambapo hadi sasa ameweza kujenga Nyumba kusomesha watoto na hata kununua magari lakini pia anauwezo wa kusaidia ndugu zake.

Amesema baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kauli mbiu ya Uchumi wa viwanda ilimuhamasisha zaidi na kufanya jitihada za kuongeza mashamba kutoka heka moja hadi kufikia 90 ambazo kati ya hizo ameshaaza kulima heka 80.

Amesema kuwa katika heka 80 amefanikiwa kupanda miti ya miparachichi 5000 ambapo kila mti mmoja kwa kadilio la chini anauwezo wakupata shilingi 200,000 kwa kila mti.

Ameongeza kuwa hivi Sasa katika uwekezaji ambao ameufanya anatarajia kupata shilingi bilioni moja kwa mwaka.

Amesema anamshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kutoa hamasa kwa watanzania hususani kwa vijana na kuwa na mafanikio makubwa aliyoyapata.

Amesema awali alikuwa akifanya shughuli za usafi kwa maana ya ufagiaji kwenye shule moja ya mtu binafsi ambapo baada ya muda alikuja kuacha na kuamua kujiajiri kupitia sekta ya kilimo.

“Hapa nataka kusema kuwa baada ya kuacha kazi na kujikita kwenye kilimo hiki Cha parachichi niliaza miti 12 na hadi kufikia mwezi wa 12 mwaka huu nitakuwa nimefikisha jumla ya miti 5000 ambayo hiyo itanipatia shilingi bilioni moja kwa mwaka”amesema na kuongeza kuwa .

“Ndugu zangu waandishi wa habari kwanza nawashukuru kwa kuja kwenu kunitembelea katika kituo hiki Nemes Green Gurden kimsingi eneo hili mnaloliona lina heka sita lakini ninajumla ya heka 90 kama nilivyowaeleza hivyo ni matarajio yangu heka hizo zitanipatia kiasi hicho cha fedha.”amesisitiza Mlimbila

***Akizungumzia zaidi uwekezaji wake katika zao la Parachichi.

Amesema kuwa ameweza kusaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana zaidi ya 50 ambao wanafanya shughuli mbalimbali za shambani.

Pia amesema amekuwa na darasa la kufundisha bure kilimo cha maparachichi kwa watu wanaopenda kujifunza.

“Nimefundisha vijana wezangu wengi sana na sasa hivi wamepata mafanikio makubwa na wenyewe wanafundisha wengine hivyo kimsingi kilimo kimenipatia mafanikio makubwa.”amesema Mlimbila.

***Akizungumzia Changamoto anazokumbana nazo.

Amesema penye mafanikio hapakosi changamoto hivyo changamoto kubwa wanayokutana nayo wao kama wakulima wa zao hilo nikuona wafanyabiara wanaotoka nchi jirani ikiwamo Kenya wanapochukua zao hilo nakwenda kwao wakiyashachakata maparachichi hayo na kuweka lebo ambayo inaonyesha kama zao hilo linapatikana nchini mwao.

Amesema Jambo hilo linawaumiza kwani parachichi la Tanzania ni zuri na lina ubora unaokidhi viwango vya soko la kimataifa .

“Tunaomba serikali kuwawezesha kuwa na viwanda vidogo vya kuchakata zao hilo ambapo watakuwa wanafanya usindikaji na kuweka nembo ya Tanzania hali ambayo itaisaidia kupandisha uchumi wa nchi,”amesema

Aidha Mlimbila akizungumzia bei amesema kuwa bei katika zao hilo si mbaya na wanapata faida.

Amesema kutokana na malighafi hiyo kupatikana kwa wingi mkoani Njombe nivema serikali pia ingeona umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya kiwanja cha ndege ili kuwawezesha wakulima wenyewe kwenda kuuza zao hilo nje ya nchi .

Amesema kwa kufanya hivyo kutaongeza thamani ya zao hilo na kuuzwa kwa bei nzuri zaidi kuliko ilivyo sasa na kuwafanya wakulima kuweza kuwa walipa kodi wazuri wa serikali .

Akizungumzia malengo yake ya baadae,amesema kuwa malengo yake ni kuona siku moja anamiliki kiwanda chake na amejipa miaka minne kuweza kufikia malengo hayo ambapo anaamini kuwa yatafikiwa kwa juhudi ambazo anazifanya.

Anasema kuwa lazima afungue kiwanda na kuja kuchakata parachichi na kuweza kusaidia wananchi na vijana wezake lakini pia anaiomba serikali kufanya mchakato ambao utawezesha wao kupata mkopo wenye riba nafuu kutoka katika mabenki.

“Nataka niwaambie kwa sisi hapa njombe kilimo cha parachichi tunakiona kama vile madini hivyo hakuna ya kuendelea kulia na umasikini wakati mkombozi upo ni shambani tu.”amesema

Anasema vijana wengi wanapenda kutembea na bahasha kutafuta fursa ya kuajiriwa lakini wanaweza kuingia kwenye kilimo ambacho kina mali kuliko kuajiliwa .

***Akizugumzia kuhusu soko la mje la maparachichi

Amesema kuwa yeye kampuni anazofanya nazo kazi ni kutoka Dubai ,Ujerumani pamoja na nchi zingine za ulaya ambako ndiko zao hilo anapowauzia.