May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Huduma za maji safi, salama zaimarika uongozi wa Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraonlineDodoma

WAZIRI wa Maji Nchini, Juma Aweso amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huduma za maji safi na salama zimeimarika kwa kiasi kikubwa kuanzia vijijini na mijini na Watanzania wamekuwa mashaidi kwa kunufaika na huduma hiyo.

Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 , Waziri Aweso amesema Chanzo kipya cha fedha kupitia Hatifungani ambapo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga imekuwa Mamlaka ya kwanza kuzindua uuzaji wa Hatifungani ya Kijani yenye thamani ya sh. bilioni 53.12.

Waziri Aweso ameongeza kuwa hadi Februari 2024, sh. bilioni 54.72 sawa na asilimia 103 zimekusanywa na fedha hizo zitatumika kuboresha miundombinu ya usambazaji maji na utunzaji wa mazingira katika Jiji la Tanga pamoja na miji ya Muheza, Pangani na Mkinga.

Pia, Wizara ya Maji imefanikisha malengo ya programu ya P for R (Lipa kwa Matokeo) kwa muda uliopangwa kwa kuvuka lengo la idadi ya wanufaika kutoka watu milioni 3 hadi milioni 4.07.

Smbamba na hayo, Waziri Aweso amesema Benki ya Dunia imeitambua Tanzania kuwa ya nchi ya kwanza kati ya nchi zaidi ya 50 duniani zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa Programu ya P for R kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo na kuongeza kuwa Mafaniko hayo yamesaidia kuongezeka kwa fedha za utekelezaji wa programu kutoka Dola za Marekani milioni 350 hadi Dola za Marekani milioni 654 na kuongeza mikoa inayonufaika kutoka 17 hadi 25 na Halmashauri kutoka 86 hadi 137.