May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aagiza Mradi Liganga, Mchuchuma uanze,azindua kiwanda cha magari

Na Irene Clemence, Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara na ya Mipango na Uwekezaji kukamilisha mchakato wa kuipata kampuni itakayowezesha kuanza kwa mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Kigamboni, jijini Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi wa kiwanda kiwanda cha kuunganisha magari makubwa cha Saturn Corporation Limited.

Kuanza kwa mradi huo uliopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe haraka kunalenga kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya kiwanda hicho, ambapo alisema zipo malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa magari ikiwemo vioo na vyuma.

“Hivyo nikuombe Waziri wa Viwanda na mwenzako wa Uwekezaji, malizieni suala la Liganga na Mchuchuma, tupate kampuni bora itakayoanza kuchimba chuma ile ili iwe malighafi katika viwanda hivi, niwaombe sasa hili limaliziwe kwa haraka,” alisema Samia.

Maelekezo hayo ya Rais Samia yanakuja wakati ambao kumekuwapo na msukumo kutoka kwa watu mbalimbali juu ya kutaka utekelezaji wa mradi huo kuanza kutokana na faida zake lukuki.

“Binafsi naiona fursa kubwa sana kwa Watanzania, tunaweza kunufaika zaidi kupitia uwekezaji wa viwanda vingine vya uzalishaji wa vipuri vya magari mitambo pamoja na kuongeza ajira na mapato kama nilivyosema mwanzo,” alisema.

Aliitaka Wizara ya viwanda kuhakikisha inaunganisha mnyororo wa thamani ili viwanda viweze kusomana, kujua nani anazalisha nini na kiwanda kimoja kinaweza kusaidia vipi kingine.

Tayari Serikali ilishatoa sh. bilioni 15.4 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi na taasisi mbalimbali 1,142 ili waweze kupisha mradi huo.

Tafiti zinaonesha uwepo wa madini hayo tani milioni 428 za makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140 na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 kinachoweza kuchimbwa kwa miaka 58. Mradi huo ni miongoni mwa ile ya kimkakati ya nchi.