May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchakataji wa madini,ubora wa vifaa ni tija kwa kipato cha juu

Na Dotto Kwilasa,Timesmajiraonline,Mwanza

WAFANYABIASHARA wa madini pamoja na jamii inayojihusha na sekta ya madini nchini wametakiwa kuhakikisha wanatumia vifaa vyenye ubora katika uchakataji wa madini ili kuongeza ubora kwa ustawi wa shughuli za madini kuendana na kasi ya maendeleo ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Nesch Mintech Tanzania Limited Happiness Nesvinga, ameeleza hayo hivi karibuni Jijini Mwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu manufaa ya uchimbaji wa madini unaozingatia ubora.

Amesema mchakato mzima wa kuanzia kuchimba mpaka kuuza madini ni mkubwa lakini jambo linaloongeza thamani yake zaidi na kumlipa mfanyabiashara ni pale ambapo madini hayo hupimwa na kuhakikiwa katika ubora wa juu na kuepuka makosa ya gharama kubwa na kudumisha ushindani.

“Huduma za maabara ni muhimu kwa mafanikio na ustawi wa operesheni za madini. Hivi ndivyo tunavyofanya kazi zetu. Nesch Mintech, tunajivunia taratibu zetu nzuri za upimaji. Tunachambua sampuli za madini katika kila hatua ya uchakataji ili kuhakikisha kuwa bidhaa ya mwisho si tu inakidhi bali inazidi viwango vya sekta. Kujitolea kwetu kwa ubora kunasaidia wateja,”amesema

Mkurugezi huyo ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi katika Kuboresha Michakato ya Uchimbaji na kampuni ya Nesch Mintech ina Maabara ambayo imejengwa na teknolojia ya kisasa ili kutoa data sahihi kwa ajili ya uboreshaji wa michakato na inasaidia makampuni ya madini kutambua njia za uchimbaji zenye ufanisi zaidi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza uzalishaji.

Amesema,Uwajibikaji wa kutunza mazingira katika shughuli za madini ni kiini cha operesheni zote na inatakiwa vipimo kamili ili kufuatilia athari za shughuli za madini, kuwasaidia wateja wetu kufuata kanuni za mazingira na kulinda sayari nzima kwa vizazi vijavyo.

Amefafanua kuwa Nesch Mintech kikiwa ni kituo cha utafiti na maendeleo ambacho mara kwa mara kinatafuta mipaka mipya katika mbinu za uchimbaji na uchakataji madini, kimelenga kuchangia katika maendeleo ya kiteknolojia katika sekta ya madini na kutathmini uwezo wa kiuchumi wa amana za madini kwa kuhakikisha faida ya miradi ya madini.

Pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiashara wa madini kuweka kipaumbele cha Usalama katika shughuli za madini ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira

“Tunapima kwa makini hatari zinazowezekana, kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi wa migodi na jamii zinazozunguka. Huduma zetu za maabara ni muhimu kwa kuunda mazingira salama ya kazi,”amesema na kuongeza,

“Nesch Mintech Tanzania Limited ni zaidi ya maabara tumekuwa ni washirika katika maendeleo na tutaendelea kuunga mkono serikali katika sekta ya uchakataji madini, kuhakikisha kuwa operesheni za madini ni zenye ufanisi, zinawajibika, na zina faida kwa kuwahakikisha utaalamu usio na kifani na msaada usioyumba, “amesisitiza.