Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Pius Chatanda (MCC), amepongeza vikundi vya wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa mafanikio yao ya kiuchumi, akisema matumizi ya mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba yamewawezesha kupanua biashara na kufikia masoko ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Chatanda alitoa pongezi hizo Agosti 4, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Songwe, ambapo aliambatana na Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, Bi. Ellen Bogohe (MNEC), Ndg. Florah Magabe, na Mbunge wa Viti Maalum. Dkt. Catherine Canute.
Alisema mikopo hiyo imekuwa kichocheo cha kuwawezesha wanawake kujitegemea kiuchumi, kupanua biashara zao na kuzalisha ajira kwa vijana, hususan katika shughuli za usafirishaji na ubebaji wa mizigo.
Chatanda alisisitiza umuhimu wa wanawake wanaorejesha mikopo kwa wakati kuendelea kupewa mikopo mipya ili kuhakikisha biashara zao haziathiriwi na ukosefu wa mtaji, hatua ambayo itaongeza tija na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha, aliwahimiza wanawake wa Tunduma kuendelea kutumia fursa za mikopo ya Serikali badala ya kukopa katika taasisi zenye riba kubwa, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wananchi kupitia utaratibu wa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Alifafanua kuwa kati ya asilimia hizo, asilimia tano hutumika kuboresha miundombinu ya wajasiriamali, huku asilimia 10 ikitengwa kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akihitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe, Chatanda alitembelea miradi mbalimbali ya UWT, kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 katika halmashauri za Tunduma, Ileje, Mbozi, Momba na Songwe, pamoja na kuzungumza na wanachama wa CCM na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na usajili wa wanachama wapya ili kuimarisha chama.

More Stories
Chatanda ahamasisha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030
UDSM yabuni bidhaa kwa nazao ya nyuki
Airtel  yaimarisha ushirikiano  wa Airtel Business Monthly Mug TournamentÂ