NA Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Buhigwe, Pius Yanda, ameishauri Serikali kuongeza fedha za utafiti katika vyuo vikuu nchini ili kuimarisha ubora wa elimu ya juu, tafiti na mchango wa vyuo katika maendeleo ya Taifa.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Profesa Yanda amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wizara kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti katika vyuo vikuu.
Amesema katika miaka iliyopita vyuo vikuu vilikuwa vikisaidiwa na Serikali pamoja na washirika wa maendeleo katika kufanikisha tafiti mbalimbali, lakini bado kuna haja ya kuwa na mkakati wa ziada wa kuhakikisha taasisi hizo zinapata fedha endelevu kwa ajili ya utafiti.
“Vyuo vina wajibu wa kufanya utafiti, kufundisha na kuchangia maendeleo ya jamii. Tunahitaji tafiti ambazo zitachangia moja kwa moja katika michakato ya maendeleo ya nchi yetu,” amesema Profesa Yanda.
Aidha, amesema changamoto ya mzigo mkubwa wa ufundishaji kwa wahadhiri imeendelea kuathiri muda wa kufanya tafiti, hususan kwa maprofesa na wahadhiri waandamizi ambao pia wanabeba jukumu kubwa la usimamizi wa wanafunzi wa shahada za kwanza, uzamili na uzamivu.
“Teaching workload ni kubwa,Wahadhiri wana kazi nyingi za kufundisha darasani na kusimamia wanafunzi. Hali hiyo inaweza kuathiri muda wa kufanya utafiti, wakati huo huo wahadhiri waandamizi wanaendelea kustaafu,” amesema.
Mbunge huyo amempongeza Rais wa Tanzania kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuajiri walimu na wahadhiri wapya, akisisitiza kuwa ajira hizo zinapaswa kuzingatia vigezo na miongozo ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Amesema ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya wahadhiri waandamizi na wale vijana ili kuondoa pengo linalojitokeza pale wahadhiri wakongwe wanapostaafu.
“Kwa vyovyote lazima kuwe na mchanganyiko wa senior na junior lecturers. Wahadhiri waandamizi wanapostaafu huleta changamoto kubwa katika ufundishaji na utafiti,” ameeleza.
Katika mchango wake, Profesa Yanda pia alitoa mfano wa ushiriki wake katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisema uzoefu huo umeonesha umuhimu wa kutumia wataalamu katika uchakataji wa taarifa za maendeleo ya Taifa.
Amesema baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo South Africa, Egypt, Ethiopia, Kenya na Rwanda hutumia mfumo wa kuteua wataalamu maalumu kuchakata taarifa za maendeleo badala ya kutegemea mifumo mirefu ya ukusanyaji wa maoni.
“Naamini hata Tanzania tunaweza kutumia wataalamu kuchakata taarifa muhimu za maendeleo kila baada ya miaka mitano ili kwenda sambamba na mahitaji ya wakati,” amesema.

More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77