Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
NAIBU Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu pamoja na masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema serikali imesikia kilio cha watu wenye ulemavu wa kusikia kuhusu ukosefu wa huduma za lugha ya alama katika maeneo ya utoaji huduma.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu lugha ya alama, amesema serikali inaendelea kuandaa sera na miongozo itakayowezesha lugha hiyo kurasimishwa rasmi nchini.
“Serikali itahakikisha mchakato huu unakamilika ili kuwapa viziwi haki yao ya mawasiliano na kupata huduma stahiki,” amesema Nderiananga.
Ameeleza kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na wizara mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo inaendelea kukamilisha mchakato huo ambao unatarajiwa kuhitimishwa hivi karibuni.
Aidha, amesema kurasimishwa kwa lugha ya alama kutahitaji uwepo wa mitaala maalumu ya kuwajengea uwezo wakalimani pamoja na wataalamu wa lugha hiyo ili kukidhi mahitaji ya jamii.
Nderiananga alisisitiza kuwa serikali inatambua mchango wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa na itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Julius Tagi, amesema kuna aina mbalimbali za viziwi katika jamii, jambo linalohitaji uelewa mpana ili kuwezesha utoaji wa huduma unaozingatia mahitaji yao.
Amefafanua kuwa baadhi ya viziwi husikia kwa kiwango kidogo na huhitaji kuzungumzewa kwa sauti ya juu au kukaa karibu na mzungumzaji, huku wengine wakiwa hawasikii kabisa hata kwa kelele kubwa.
Pia alisema wapo waliozaliwa na uziwi tangu kuzaliwa na wengine waliopoteza uwezo wa kusikia ukubwani kutokana na magonjwa au sababu nyingine, ambapo baadhi yao wana uwezo wa kuzungumza lakini hawawezi kusikia.
“Jamii inapaswa kuelewa tofauti hizi ili iwe rahisi kuwahudumia na kuwasiliana nao kwa njia sahihi,” amesema Dkt. Tagi.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Selina Mlemba, amesema semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wabunge ili kusaidia kutungwa kwa sera na sheria zitakazolinda haki za viziwi.
Amesema kwa sasa hakuna sheria inayowalazimisha watoa huduma kuwa na wakalimani wa lugha ya alama katika maeneo yao.
Selina alitaja maeneo muhimu yanayohitaji huduma za wakalimani kuwa ni hospitali, vituo vya polisi, vituo vya usafiri na vituo vya televisheni.
“Viziwi wanahitaji lugha ya alama irasimishwe ili waweze kupata haki yao ya mawasiliano kama wananchi wengine,” almesema.

More Stories
Wizara,TPSF kuongeza ushiriki kongamano la kiswahili
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini