March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu awataka mabalozi kuvutia wawekezaji

Na Mwandishi wetu, TimesMaajira Online

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali watoe msukumo Katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi, kuimarisha biashara pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika maeneo yao ya uwakilishi.
 
Pia, Waziri Majaliwa amewasisitiza mabalozi hao kuhakikisha wanalinda taswira ya Tanzania katika nchi za uwakilishi sambamba na kujielekeza katika kuvutia watalii na kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kufanya biashara nje.
 
Waziri Mkuu amekutana na mabalozi hao leo (Jumatatu, Januari 17, 2022) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. Mabalozi aliyokutana nao ni Balozi Profesa Adelardus Kilangi (Brazil), Balozi Said Juma Mshana (DR-Congo), Balozi Alex Gabriel Kalua (Israel), Balozi Said Shaib Mussa (Kuwait) na Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta (Urusi).
 
Kadhalika, Waziri Majaliwa amewataka mabalozi hao wahakikishe wanakwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa balozi kwa kubana matumizi hususani katika mambo yasiyokuwa ya lazima. “Pia mkaimarishe mahusiano kati yenu na maafisa wa ubalozi.”


 Pia, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakutane na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na wawasaidie kuimarisha Jumuiya zao kwa kuwa na uongozi imara. “Waunganisheni ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na kwenye shughuli za kijamii mnazozifanya huko.”
 
Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wanatakiwa kuitangaza sana lugha ya Kiswahili. “Naamini mkitumia ushawishi wenu katika kukitangaza Kiswahili kinaweza kuwa chanzo cha ajira kwa Watanzania nje hususan kwa walimu wa fani hiyo sambamba na kuitangaza nchi yetu.”