April 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Jafo atoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira Suleiman Jafo ameelekeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchi nzima kuanza kusimamia kampeni katika wilaya zote 139 nchini kwamba kila mwanafunzi wa shule ya msingi, sekondari na chekechea awe na mti wake alioupanda na kuusimamia kwa mwaka mzima.

Pia Waziri Jafo ameelekeza maeneo yote nchini kuwa agenda ya usafi siku ya jumamosi iendelee kwani jambo hilo limeonekana kusahaulika.

Waziri Jafo ametoa maelekezo hayo katika ziara yake aliyoifanya Mkoani Tanga wakati akipanda mti wa mfano katika ofisi za misitu jijini Tanga ikiwa ni muendelezo wa ziara yake inayogusa mikoa 11 nchini.

Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini walisimamie jambo hilo katika maeneo yao kwamba kila mwanafunzi awe wa msingi, sekondari au chuo awe anamiliki mti mmoja aliouotesha na kuweza kuusimamia ndani ya mwaka mzima.

“Katika ziara yangu hii nimetembelea taasisi mbalimbali hususani shule za msingi na kuendesha kampeni ya kuanza kupanda miti imani yangu kwamba suala la upandaji wa miti itakuwa ni elimu inayoanza kwa watoto wadogo walioko mashuleni na jambo hili litakuwa endelevu hivyo zoezi hilo la kupanda miti, “alisistiza Waziri Jafo.

“Zoezi la kupanda miti katika kila taasisi ama mtu yeyote aitwaye mwanafunzi lazima apande mti wakecmmoja na kuusimamia mti huo hiyo ni tofauti na programu ya kuhakikisha kwamba kila halmashauri inapanda miti milioni 1.5 inawezekana ndani ya idadi hiyo lakini pia itachangiwa na idadi ya wananfunzi waliopo kwenye maeneo husika, “amebainisha waziri Jafo.

Waziri Jafo amesema anatarajia Tanga itakuwa ya mfano katika zoezi hilo na kueleza kuwa agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan mmemsikia katika vikao mbalimbali vya kitaifa na kimataifa kwamba jambo kubwa alilosisitiza ni agenda ya mazingira lakini pia hata katika mikutano yake ya ndani amekuwa akisistiza suala hilo yeye pamoja na makamu wa Rais.

“Niwatake watu wote wa Tanga na maeneo mengine twendeni tukasimamie agenda ya mazingira kwanguvu zote tukijua wazi mabadiliko ya tabia nchi sasa yamekuwa dhahiri na wazi sisi wenyewe tuna kila sababu ya kusimamia hayo mabadiliko ya tabia nchi tweze kuyasimamia vizuri, “amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi hivi sasa iko wazi na kiwango cha joto kimeongezeka hivyo suala la ukame limeshamiri na kupelekea baadhi ya wanyama kufa kutokana na ukame na hii ni kutokana na ukosefu wa mvua.

Hivyo kutokana na hali hiyo waziri Jafo amesema kila Halmashauri inapaswa kupanda miti milioni 1.5 kwa lengo la kupata miti milioni 276 kwa mwaka hali itakayosaidia kuwa mkombozi wa kupata mvua zinazotabirika katika maeneo mbalimbali.

Katika hatua nyingine waziri Jafo ameelekeza maeneo yote nchini kwamba agenda ya usafi haina mjadala hivyo viongozi katika maeneo yote wanapaswa agenda ya kwanza wanapoamka asubuhi maeneo wahakikishe maenwo yanakuwa masafi wakati wote ikiwa ni pamoja na kuzingatia kwamba siku ya, jumamosi ni siku ya kufanya usafi katoka maeneo yote.

“Katika eneo hilo nielekeze majiji yote na, manispaa zote ndani ya Tanzania katoka ziara yangu hii itakayogusa mikoa 11niwaelekeze kwamba agenda ya usafi haina mjadala kama maenelekezo aliyoyatoa mh Rais na Makamu wa Rais agenda ya usafi ipewe kipaumbele, “amesisitiza Waziri Jafo.

Wakati huo huo waziri Jafo alimpongeza, mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya kwamba ni mwenyekiti wa mfano na timu yake katika usimamizi mzuri anaouganya katika nyanja mbalimbali.

Aidha Waziri Jafo aliipongeza Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kupata namba moja katika Usafi huku akisema kuwa namba moja hiyo sio kwa kupendelewa bali ni ukweli kwamba wanastahili.

“Naomba niwasifu Tanga mnafanya vizuri sana kwa usafi nyinyi hamfanani na wale wengine ambao ni makao makuu ya nchi ambapo makamu wa Rais alipita na kukuta jiji hilo ni chafu kwakweli mnastahili sifa jiji la Tanga endeleeni na uamaduni huu huu wa kuhakikisha Tanga inakuwa safi.
,”alisema Waziri Jafo.

Habari picha ni Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jafo akipanda mti wa mfano jijini Tanga ambapo alisisitiza wakuuu wa mikoa na wilaya nchini kusimamia zoezi la upandaji wa miti kwa wanafunzi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Picha ma Hadija Bagasha Tanga