April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Manispaa ya Moshi yaongeza ukusanyaji mapato kufikia Bil 8.5

Na Martha Fatael, TimesMajiran Online, Moshi

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imeongeza makusanyo ya ndani kutoka shilingi Bil. 6.4 mwaka wa fedha 2021/2022 na kufikia Bil 8.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Kadhalika halmashauri hiyo imepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ya zaidi ya Bil 50.3 ikiwa inajumuisha ruzuku kutoka serikali kuu zaidi ya Bil 42 na makusanyo ya halmashauri hiyo zaidi ya Bil. 8.5.

Akiwasilisha hoja ya makadirio hayo, mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Juma Raibu, amesema makusanyo hayo yameongezeka ikiwa ni baaya ya kuongeza maeneo mapya ya ukusanyaji mapato hayo.

Amesema bajeti hiyo imezingatia miongozi ya serikali ambapo asilimia 60 imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ambapo kiasi Cha zaidi ya Bil 7 kimetengwa, huku asimia 10 ya mikopo kwa wanawake na vijana ikiwekwa.

“Tunapoteza mapato bado…..kwa miaka ijayo Manispaa tunauwezo wa kuongeza ukusanyaji ikiwa matukio ya harusi yatafuatiliwa na kukusanya mapato kama ya washereheshaji(MC), wapishi na huduma nyingine katika matukio hayo” amesema

Akichangia katika kikao hicho, mbunge wa Jimbo la Moshi, Priscus Tarimo amewataka watendaji na madiwani kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo katika kukamilisha miradi ya maendeleo iliyokwisha kuanza miaka iliyopita.

Aidha mbunge huyo amewaasa watendaji kufanya ukusanyaji wa mapato wa kirafiki badala ya ule wa kushurutisha kwani unasababisha kutokusanya fedha zilizokusudiwa, ambapo amewataka kuanza kwa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kutoa mapato kwa hiari.

Awali diwani wa kata ya Mjimpya, Abuu Shao, diwani wa kata ya Kiboroloni Frank Kagoma na diwani wa Shirimatunda Francis Shio wamesema wapo tayari kutoa ushirikiano kwa watendaji katika ukusanyaji mapato huku wakipongeza ushirikiano wakati wa uandaaji bajeti na kwa meya kwa usimamizi wa bajeti Bora iliyopitishwa.

Hata hivyo mbunge wa viti maalum, Zuwena Bushiri ameomba ushirikiano zaidi kwa watendaji na wananchi wa Manispaa hiyo katika kuendelea utamaduni wa kupata tuzo ya usafi wa mazingira kwani ni kwa manufaa ya jamii hiyo.