April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkenda akabidhi matrekta yaliyonunuliwa kwa mkopo wa TADB

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Mbarali

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amekabidhi zana za kisasa 15 za kuvunia mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya zenye thamani ya sh. milioni 950.

Zana hizo hizo zimenunuliwa kwa mkopo toka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Akikabidhi matrekta hayo ya kisasa yenye zana za kuvunia mpunga kwa Chama cha Msingi cha Nguvu Kazi ya Wanavala, Waziri Mkenda alisema zana hizo zina manufaa makubwa kwa sababu zinakwenda kunufaisha zaidi ya wakulima 5,000 katika Wilaya ya Mbarali na maeneo jirani.

“Kilimo cha mpunga ni zao la pili nchini kulimwa zaidi baada ya mahindi. Changamoto katika kilimo cha zao hili imekuwa ni pamoja na zana duni za kilimo, mbegu na pembejeo nyingine.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda katikati akikabidhi mfano wa hundi ya Milioni 950 iliyotolewa na benki ya Kilimo ( TADB) kwa wakulima katika kijiji cha imalilosongwe kilichopo kata ya Ubaruku wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya, Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Japhet Justine, wapili kulia ni Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Nguvu Moja Bw. Hamza Tamimu na watatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbalali Bw. Reuben Mfune.

Nifaraja kwangu kukabidhi zana hizi ikiwa ni sehemu ya kuleta chachu na mabadiliko katika sekta ya kilimo. Kwa zana hizi mnakuwa na uhakika wa kuvuna kwa wakati na hivyo kupunguza upotevu wa mazao yenu,” amesema Profesa Mkenda.

Waziri huyo pia ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kazi nzuri inayofanya katika kuchagiza mageuzi kwenye sekta ya kilimo hapa nchini:

“Zana hizi za kuvunia ni ushahidi tosha kuwa mchango wa TADB katika sekta ya kilimo ni mkubwa na unalenga kuchochea na kuleta maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo,”amesema.

Profesa Mkenda pia amewataka wakulima kuhakikisha wanatumia ipasavyo mashine hizo pamoja na kuzitunza sambamba na kuimarisha utendaji kazi wa mashine hizo ili zilete tija kwenye uzalishaji wa mpunga kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Japhet Justine amesema kwamba mikopo ya matrekta ya kulimia na kuvunia pamoja na zana nyingine za kilimo zimetolewa kupitia program ya ushirikiano kati ya TADB na kampuni ya John Deere na LonAgro kwa makubaliano ya utoaji wa mikopo ya riba nafuu na isiyozidi asilimia 12 kupitia ruzuku inayoitwa ‘interest buy down’ ambayo inampa mkulima ahueni katika riba ya mkopo.

Akielezea zaidi mpango wa zana za kisasa unaofanywa na TADB, Justine alisema kuanzia mwaka 2017 hadi sasa, zaidi yakiasi cha sh. Bilioni 12 za mikopo imetolewa katika ununuzi wa zana za kisasa za kilimo.

Kati ya hizi sh. Bilioni 8.3za mikopo imetolewa moja kwa moja na TADB katika ununuzi wa zana za kisasa za kilimo 123. Ambapo zana za kulimia ‘Matrekta’ ni 90 na zana za kuvunia ‘Combined Harvester’ ni 19, idadi inayobaki ni zana kama ‘planter’ na ‘plough’.

Zana hizi zimenufaisha moja kwa moja wakulima 5,800 katika mikoa ya Katavi, Manyara, Pwani, Kagera, Mwanza, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Tanga na Zanzibar.

Wakati huo huo, sh. Bilioni 3.7 pia imetolewa katika ununuzi wa zana za kisasa za kilimo kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS), ambayo imewezesha jumla ya zana za kisasa 76. Hivyo kufikisha jumla ya uwekezaji katika zana za kisasa za kilimo kufika Shilingi Bilioni 12.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda katikati akisalimiana na mmoja wawanufaika wa mkopo wa mashine ya kuvunia mpunga ‘’ combine harvesters’’ Bi. Sara Mgeni wakati wa Hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi ya Milioni 950 iliyotolewa na benki ya Kilimo ( TADB) kwa wakulima katika kijiji cha imalilosongwe kilichopo kata ya Ubaruku wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya, wapili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Japhet na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbalali Bw. Reuben Mfune.

Akitoa taarifa ya uwekezaji wa TADB katika kanda hiyo, Justine alisema, “Hadi kufikia Juni 8, 2021, TADB ilikuwa imeshatoa mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 23.3 ambayo imenufaisha wakulima 14,508 katika mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini,”

Akifafanua zaidi alisema; “Kati ya kiasi hicho, mikopo ya sh.bilioni 13.9 imetolewa kama mikopo ya moja kwa moja na sh. bilioni 9.4 imefanikishwa kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS) unaowezesha wakulima na SME za kilimo kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za fedha kwa udhamini wa TADB.

Minyonyoro ya thamani iliyoguswa katika mpango huu ni zao mpunga, mahindi, kahawa, mboga mboga, mtama, chai na ufugaji wa kuku.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Nguvu Kazi ya Wanavala, Hamza Tamimu aliishukuru TADB kwa kuwawezesha kupata matrekta kwani yatachochea kilimo cha mpunga.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda kulia akiliwasha moja ya mashine ya kuvunia mpunga ‘’ combine harvesters’’ kwenye hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi ya Milioni 950 iliyotolewa na benki ya Kilimo (TADB) kwa wakulima katika kijiji cha imalilosongwe kilichopo kata ya Ubaruku wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya, Wa pili kulia ni mmoja wa wakulima alienufaika na mkopo huo, Sara Mgeni, wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbalali, Reuben Mfune na watatu kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine.

“Napenda kuishukuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kututhamini sisi wakulima wadogo kwa kutupa mkopo wa zana za kisasa za kuvunia mpunga ambayo zitaenda kuongeza uzalishaji, kwani tutavuna kisasa na kuongeza tija katika zao la mpunga ,” amesema Tamimu.