April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Chande: Uharibifu wa misitu umekuwa mkubwa na kutishia usalama

Na Robert Hokororo,TimesMajira Online, Mbeya

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande amesema uharibifu wa misitu nchini umekuwa ni kubwa na hivyo kutishia usalama wetu.

Chande amesema hayo juzi alipokuwa akizungumza wakati akizindua Mradi wa “Urejeshwaji endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai” iliyofanyika jijini Mbeya.

Amesema tafiti zimebainisha kuwa kila mwaka nchi yetu hupoteza wastani wa takriban hekta 469,420 za misitu na upotevu huo umesababisha upotevu mkubwa wa bioanuai na hatari ya kutoweka kwa baadhi ya aina muhimu za jamii ya mimea na wanyama.

“Kama kasi ya uharibifu wa mazingira isipodhibitiwa, nchi yetu itakuwa katika hatari ya kugeuka jangwa kwa mfano tathmini iliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii imeonesha hali ya uharibifu ikiendelea hivyo, katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2033, uharibifu wa misitu utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 167 za kurejesha mazingira katika hali yake. Kiasi hiki kingeweza kufanya shughuli za kimaendeleo katika taifa letu kama tutatunza mazingira vizuri,” amesema Chande.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Hassan Chande akizungumza wakati wa warsha ya kuzindua mradi wa ‘Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira.

Naibu Waziri Chande ameongeza kuwa nchi yetu inakadiriwa kuwa na hekta millioni 48.1 za misitu sawa na wastani wa asilimia 51 ya eneo lote la nchi kavu ambayo ina manufaa makubwa katika hifadhi ya bionuai ikiwemo makazi ya viumbe hai, vyanzo vya maji, husaidia kupunguza joto ukaa na zaidi ni husaidia kutunza ardhi yetu kuwa na rutuba.

Aidha, aliwakumbusha kuwa Serikali haitavumilia kuona ubadhilifu wa aina yoyote katika utekelezajiwa mradi huu na kwua Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha thamani ya fedha inaendana na miradi itakayotekelezwa katika maeneo yetu.

Awali akitoa neno la ukaribisho, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga amebainisha kuwa Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 11.2 sawa na sh. Bilioni 25.7.

Amesema lengo la mradi huu ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo-ikolojia na jamii kwa ujumla na ni sehemu ya mradi mkubwa wa kidunia (The Global Groject) unaotekelezwa katika nchi 11 duniani ikiwemo Tanzania.

Maganga alishukuru GEF na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kushirikiana na Serikali kupata fedha za utekelezaji wa mradi huu pamoja na Shirika la IUCN kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika hatua zote za maandalizi ya mradi.