April 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa maendeleo nchini waombwa kuunga mkono juhudi za utoaji elimu ya lishe

Na Yusuph Digossi

Wadau wa maendeleo nchini wameombwa kujitokeza kuunga Mkono Juhudi za maendeleo kwa jamii kwa kuleta Suluhu za matatizo yanayoikabili ikiwemo kutoa mafunzo ya lishe bora na ulaji unaofaa kwa watoto na vijana.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi na mwanzilishi wa Taasisi ya Tanzania Nutrition Connect (NCT) Jackline Kawiche wakati wa utoaji wa elimu ya lishe na mtindo bora wa maisha kwa watoto kwa watoto uliofanyika katika shule za msingi Luguruni na Kwembe zilizopo, Mbezi Luguruni Manispaa ya Ubungo, yenye lengo la kuwafundisha watoto kuhusu elimu ya lishe bora, mtindo bora wa maisha na ulaji unaofaa ili kujikinga na Magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza na TimesMajira Mkurugenzi huyo amesema lengo la kutoa elimu hiyo kwa watoto ni kuwajengea msingi mzuri wa lishe na mtindo bora wa maisha kwasababu njia ya kuwekeza kwa watoto ni bora zaidi katika msingi wa maisha ya baadae.

” Leo tumekuja hapa katika shule ya msingi Luguruni , kwaajili ya kutoa elimu ya lishe na mtindo bora wa maisha kwa watoto wa darasa la pili, kwasababu tumeona kwamba tukiwekeza kwa watoto itasaidia kujenga msingi mzuri wa masuala ya lishe na kuwakinga watoto na kupunguza vifo huko baadae” Amesema Kawiche

Amesema katika utafiti mdogo waliofanya wamebaini kuna changamoto ya ulaji kwa watoto haswa wanapokuwa mashuleni wanapenda kula vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi,na kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiombukiza kama vile kisukari, presha na magonjwa ya moyo.

“Baada ya kuligundua hili tukaona kuna haja ya kuja kwenye mashule kuweza kuwaelimisha watoto kuhusu ulaji ulio sahihi kwa kutumia vyakula vya asili vinavyopatikana katika mazingira yetu kama vile matunda na mbogamboga” amefafanua Jackline Kawiche

Ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kuwajengea utamaduni wa kupenda kula vyakula vya asili ili kuwajengea msingi bora wa lishe na mtindo mzuri wa maisha kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho .

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa taasisi ya Breast Feeding , Idda Katigula ambaye anashirikiana na taasisi ya ‘Nutrtion Connect’, ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi hizo ili kujenga Taifa bora litakalokuwa na vijana wenye afya na mtindo bora wa maisha.

“Nichukue fursa hii kutoa wito kwa watanzania na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za kuijenga Tanzania itakayokuwa na vijana wenye misingi bora ya afya” Amesema Idda

Naye Gerald Lymimo ambaye ni mratibu wa mpango wa maziwa mashuleni kutoka kampuni ya’ Asas Diaries Limited’ amesema wameamua kuungana na Taasisi ya Nutrition Connect , ili kufanya tathmini na kuona wanafunzi wanavyoishi na vyakula wanavyokula pamoja na kuhamasisha unywaji wa maziwa kwasababu kuna uhusiano mkubwa kati ya ufaulu wa mwanafunzi na unywaji wa maziwa.

‘Nutrtion Connect Tanzania’ ni taasisi inayoundwa na wataalamu wa lishe ambayo imejikita katika utoaji elimu ya lishe na mtindo bora wa maisha kwa lengo la kuzuia magonjwa yasioambukiza kama vile kisukari,presha,na magonjwa ya moyo.