April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea ubunge Jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga (katikati) akiwa na wazee wa kimila akisubili kusimikwa

Wazee wa kimila wamsimika mgombea ubunge Kalenga

Na Zuhura Zukheir, Iringa

WAZEE wa mila ya wahehe mkoani Iringa wamemsimika mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jackson Kiswaga ikiwa ni ishara ya kumbariki katika nafasi anayoiomba ya kuwatumikia wakazi wa jimbo la Kalenga katika nafasi ya ubunge.

Wakizungumza wazee hao kwa niaba ya chifu wa wahehe Adam Sapi Mkwawa wa pili wakati wa zoezi la kumsimika lililofanyila katika viwanja vya Ngome ya Lipuli eneo la Kalenga wamesema kuwa shughuli ya kusimikwa haifanywi kiholela ni lazima chifu wa wahehe atoe kibali ambacho hutolewa baada ya kujiuliza kwa Mutwa Mkwavinyika ambaye ndio chifu wa wahehe wa kwanza.

Mgombea ubunge Jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga (katikati) akiwa na wazee wa kimila akisubili kusimikwa. Picha zote na Zuhura Zukheir

Shughuli ya kumsimika Kiswaga ilifanyika wakati wa uzinduzi wa kampeni katika Jimbo la Kalenga ambapo Kiswaga alitoa shukrani zake kwa wazee wa mila ya wahehe walofika katika uzinduzi wa kampeni na kusema kuwa imani aliyopewa na wahehe wa Kalenga ni kubwa hivyo ana deni la kuhakikisha maendeleo yanaenda kasi katika jimbo hilo ambalo limekuwa na historia kubwa ndani na nje ya nchi.

Alisema kuapishwa na wazee wa kimila ni ishara tosha ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka huu na kuwataka wananchi na wanaCCM wasirdhike na ishara ya ushindi inayoonekana bali wajitokeze kwa wingi kupiga kura za Rais,mbunge na madiwani wote wa CCM bila kuchanganya.

Kiswaga alisema jimbo la Kalenga linakabiliwa na changamoto nyingi kama kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara baada ya mvua nyingi kunyesha, changamoto ya mimba kwa watoto wa shule kutokana na shule nyingi kutokuwa na mabweni, umeme baadhi ya vijiji changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ya uhakika pamoja na umeme kwa baadhi ya vijiji.

Alisema kama wananchi watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao atahakikisha anaenda kuzishughulikia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vijana wanawake na makundi yenye walemavu wanajiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka kupitia mfuko wa halmashauri.

Akizungumzia kuhusu barabara kuu ya Iringa kuelekea Hifadhi ya Ruaha Kiswaga alisema tayari Serikali imeshakamilisha upembuzi yakinifu hivyo inakwenda kuanza ujezi wake wanachotakiwa wananchi kuendelea kuwa na Imani na CCM kwa kupigia kura nyingi kuanzia Rais mbunge na madiwani.

Akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Abel Nyamahanga amewata wananchi kujitokeza kupiga kura kwa Rais kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati.

Alisema Serikali imedhamilia kuondoa umasikini kwa wananchi wake ndio maana imeanza kwa kutoa elimu bila malipo, kusogeza karibu huduma ya afya kwa kuongeza vituo vya afya hivyo kutokana na mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM ni wajibu watanzania kumzawadia mgombea urais wa chama hicho kwa kura nyingi za kishindo.

Aidha Mwenyekiti wa Ccm Nyamahanga baada ya kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Kalenga alimkabidhi ilani ya uchaguzi na kumtaka aisome na afanye kazi ya kuwatumikia wananchi kama ilani ya Ccm inavyoelekeza.

Alisema CCM ni chama kinachoaendeshwa kwa demokrasia ndio maana hata uongozi wake unabadilishana na baada ya kubadilishana hata ambao hawakupitishwa wanaunganisha nguvu zao na kuwa kitu kimoja

Mjumbe wa mkutano mkuu taifa MNEC kutoka Iringa vijijini Alif Abri alisema tathmini inaonesha asilimia 85 ya kura ni za CCM kutokana na Serikali kufanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Abri alisema kutokana na kazi kubwa ya Serikali chini ya Dkt. John Magufuli wananchi wanatakiwa kumpigia kura nyingi zitakazoifanya wilaya hiyo kuwa kinara kwa watakaompigia kura za urais.

Alisema katika ubunge hana shaka na wakazi wa Kalenga kwa kuwa wanatambua Kiswaga ni mtu amabaye tayari alishaanza kufanya maendeleo katika jimbo kabla hata kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Alisema wakazi wa Kalenga wanatakiwa kuchagua mafiga matatu yaani mbunge, diwani na Rais wa ccm wasije changanya kama ilivyokuwa awamu iliyopita kwa baadhi ya kata.

Wengine waliomuombea kura mgombea wa nafasi ya Rais,mbunge na madiwani ni wabunge wa viti maalum ambao ni wateule Rose Tweve, Rita Kabati, Nance Nyalusi, wengine ni Zainab Mwamwindi na mke wa Mgombea ubunge Mama Monica Kiswaga ambao wote kwa pamoja wameomba kukipigia kura chama cha mapinduzi CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge pamoja na urais.