April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afungwa miaka 30 kwa ubakaji

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Singida

MKAZI wa Kijiji cha Bukatika, Kata ya Matongo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Shabani Salimu(25) amehukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 13.

Mwanasheria wa serikali, Elizabeth Barabara amedai katika shauri la jinai namba 135/2019, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni,16,2019 saa 9:00 mchana kwenye kijiji hicho cha Bukatika.

Mwanasheria huyo amedai, siku ya tukio binti huyo alikuwa ameenda kutafuta kuni na wakati akirejea nyumbani alikutana na mshitakiwa ambaye alimvuta na kumwingiza vichakani na kisha kumbaka.

Kwa mujibu wa Barabara wakati binti huyo alipokuwa akivutwa kupelekwa vichakani, alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada kwa wasamaria wema lakini haikuwezekana kupata msaada kutookana na eneo hilo kuwa mbali kidogo na makazi ya watu.

Mwanasheria huyo amedai kuwa, katika maelezo yaliyotolewa na mshitakiwa kituo cha Polisi alikiri kumtendea unyama binti huyo na alipofikishwa Mahakamani alikana kuwa hajamtendea chochote binti huyo.

Lakini baada ya mshatakiwa Shabani kukataa kutenda kosa hilo, upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi 10 ambao waliyoa ushahidi usiokuwa na shaka yoyote kuwa mshitakiwa ndiye aliyembaka binti huyo na ndipo Mahakama ilipomtia hatiani.

Kabla ya kutoa hukumu kwa mshitakiwa huyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Robert Oguda amesema, vitendo vya ubakaji katika jamii vimezidi kushika kasi jambo ambalo linaweza kuchangia ongezeko la magonjwa yatokanayo na kujamiana.

Kufuatia hali hiyo Hakimu Oguda amesisitiza kuwa, ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya mshitakiwa huyo, Mahakama hiyo imemuhukumu Shabani Salimu adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.