Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani watu wawili ambao ni mlinzi (baunsa) na mfanyakazi wa usafi waliokuwa wakifanya kazi katika baa ya Las Vegas, wakituhumiwa kwa mauaji ya Mzafuru Yunusu mkazi wa Mwanza aliyekuwa mteja katika baa hiyo.
​Washtakiwa hao ni Yohana Peter (22), ambaye ni mlinzi wa eneo lilipotokea tukio hilo na Hamis Mussa (27), mfanyakazi wa usafi,ambapo wawili hao wamepandishwa kizimbani leo Alhamisi Mei 14, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kusomewa shtaka la mauaji.
​Akisoma shauri hilo la jinai namba 10492 la mwaka 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Christian Mwalimu, Wakili wa Serikali Clara Muhando, akisaidiana na Evance Kaiza, ameieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo, Februari 5,2026 katika baa ya Las Vegas iliyopo eneo la Kona ya Bwiru, mtaa wa Nyamanoro, wilayani Ilemela.
​Washtakiwa wote wawili, wakiwa katika baa hiyo ya Las Vegas, wanadaiwa kumshambulia na kumuua Mzafuru Yunusu kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
​Hata hivyo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza mashauri ya mauaji.
​”Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili, kwa hiyo hamtatakiwa kujibu chochote juu ya tuhuma zenu,kesi inayowakabili haina dhamana, hivyo mtaendelea kuwa mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika,”amesema Mwalimu.
​Huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Mei 28, 2026, na washtakiwa wamerejeshwa rumande.

More Stories
TAKUKURU Kinondoni yaainisha mafanikio Januari_ Machi 2016
Serikali yafikisha Umeme Katika Migodi 289 ya Wachimbaji Wadogo
Vipaumbele tisa bajeti Maliasili na Utalii