May 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil.16 kukamilisha ujenzi hospitali ya Mwl Nyerere Musoma

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Mara

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, iliyopo katika Kata ya Kwangwa, Wilaya ya Musoma mkoani mara.

Ikiwa ni siku ya kwanza kwenye ziara yake mkoani Mara, leo Mei 14, 2026 pia Kihongosi amekagua miradi ya TACTIC inayohusisha soko la Nyasho, Stendi ya Mabasi ya Mkoa iliyopo katika eneo la Bweri, na barabara ya Musoma Bus hadi kwa Saa Nane na Shaban hadi Mukendo katika Manispaa ya Musoma.
‎
Hospitali hiyo ambayo ujenzi wake uliasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere mwaka 1975, licha ya kuanza kutoa huduma lakini unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mkandarasi kutolipwa hali iliyosababisha ucheleweshaji wa mradi, na upungufu wa watumishi.


‎
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Osimund Dyegura amesema, tangu mwaka 2021, wameshatumia Sh. Bil 32 katika ujenzi wa majengo, ununuzi na ufungaji wa vifaa vya matibabu na magari ya kubebea wagonjwa.
‎
Amesema kwa sasa ujenzi wa hospitali hiyo uko kwenye awamu ya tano unaohusisha ujenzi wa kituo cha damu salama kwa Sh. Bil 1.8, kununua vifaa na kufunga umeme wa njia kubwa, huku mkandarasi akiwa ameshalipwa Sh. Bil 4 pekee kati ya Sh. Bil 40 anazopaswa kulipwa.
‎
Amesema kwa sasa hospitali hiyo inahudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 500 kwa siku, jambo ambalo linafanya mahitaji ya wataalam kuwa makubwa.


‎
“Tunazo changamoto mbalimbali tuna wagonjwa wengi baada ya kuanza kutoa huduma lakini eneo la mradi yakiwemo majengo yaliyokamilika ni dogo, tunaomba spidi (kasi) ya mkandarasi iongezeke na malipo yake yakamilike. Vilevile, tuna uhaba wa watumishi japokuwa siyo tatizo kubwa sana,” alisema Dk. Dyegura
‎
Kwa mujibu wa Dk. Dyegura, wazo la ujenzi wake lilianza 1975 na ujenzi kuanza rasmi 1980, awamu ya pili ukaendelea mwaka 2007 kwa Sh. Bil 12.4, awamu ya tatu mwaka 2008 kwa Sh. Bil 1.7 kisha ujenzi ukasimama hadi mwaka 2018 na kuanza kujengwa tena mwaka 2019 kwa Sh. Bil 7.4.
‎
Akizungumzia changamoto hizo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema mradi huo ni moja ya miradi mikubwa nchini na katika kuhakikisha unakamilika na kutoa huduma stahiki, katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga Sh. Bil 16, ambazo anaamini zitatatua changamoto iliyopo.
‎
Amesema kwa sasa hospitali hiyo inao watumishi 600, huku upungufu ukiwa ni watumishi 100, ambapo changamoto hiyo ataifikisha kwa Waziri wa Afya ili kuipatia ufumbuzi.
‎
“Maana yake mradi utakamilika, kinachohitajika ni usimamizi makini. Nimeambiwa mkandarasi anadai fedha, hili naomba nilibebe na nitalifikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kumwambia kuwa Mara wana changamoto hii,” amesema Kihongosi.


‎
Pia ameongeza “Mradi huu ni fikra za Baba wa Taifa, kukamilika kwake maana yake tutakuwa tumeziishi fikra zake. Naamini hii kazi Rais Samia Suluhu Hassan atakwenda kuikamilisha kabla hajaondoka madarakani,” alisema.