Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza
WATANZANIA wameshauriwa kuacha tabia ya kutumia dawa bila kumuona mtaalamu wa afya (daktari) pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya dawa ili kuepuka tatizo la vimelea sugu vya dawa.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa dhidi ya vimelea sugu vya dawa, watu milioni 10 watapoteza maisha ifikapo mwaka 2050 kutokana na tatizo hilo. Kwani, tathmini iliyofanywa mwaka 2019 ilionesha uwepo na vifo vya watu takribani milioni 1.27, ambavyo vilisababishwa moja kwa moja na vimelea sugu vya dawa, huku idadi hiyo ya vifo ikitajwa kuwa kubwa ikilinganishwa na watu waliokufa kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) au malaria.
Akizungumza na TimesMajira Online Septemba 23,2026 ofisini kwake, Msaidizi Mkuu wa Idara ya Pharmacy katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mfamasia Tabibu Maganga Gabriel amesema,jamii inapaswa kuacha kutumia dawa zilizopita muda wake pamoja na kutotumia dawa tofauti na muda ulioelekezwa.
“Na hapa wakati mwingine sisi wataalamu tunakosea,unakuta unamwelekeza mtu ameze dawa mara tatu kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni, bila kueleza kuwa ni baada ya saa ngapi. Hivyo, ni wajibu wa mgonjwa kuhakikisha ameelewa na kufuata maelezo, na ikitokea changamoto basi atoe taarifa kwa mtaalamu au kituo cha afya kilicho karibu,” amesema Gabriel.
Gabriel amesema,wafamasia wana mchango mkubwa katika kupambana na matumizi holela ya antibiotiki (antibiotics), pamoja na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa na kutotumia dawa kabla ya kumuona daktari au mtaalamu wa afya.
“Wafamasia tumekuwa tukifuata miongozo ya kuzuia kupata na kusambaa kwa vimelea kupitia ‘IPC’, pamoja na kufuata sheria na kanuni za kitaaluma,”amesema Gabriel.
Amesema,usugu wa vimelea unaongoza kwa vifo duniani kuliko baadhi ya magonjwa, lakini kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando bado haijafanya utafiti wa namna gani tatizo hilo linasababisha vifo kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.
Pia amesema,upungufu wa wafamasia hapa nchini ni moja ya changamoto inayoikabili sekta hiyo, hali ambayo inachangia kushindwa kutimiza majukumu yao kwa usahihi.
“Mfano, kila wodi inatakiwa kuwa na angalau wafamasia wawili. Je, kwa hapa Bugando tu tuna wodi ngapi? Bado wale wagonjwa wa nje wanahitaji dawa. Hivyo, kutokana na uchache huo, inaweza kusababisha huduma isiyo sahihi. Ombi langu kwa Serikali iajiri wafamasia wengi ili kutoa huduma bora na sahihi kwa wananchi,”amesema Gabriel.
Sanjari na hayo,amewahimiza wafamasia kukumbuka kiapo chao cha kulinda afya za wananchi kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wanapoelekea katika maadhimisho ya Siku ya Wafamasia Duniani, ambayo hufanyika kila ifikapo Septemba 25 ya kila mwaka. Kwa mwaka huu, kauli mbiu inasema, “Kuwawezesha Wafamasia kwa Kesho Yenye Afya.

More Stories
Madereva guta 72 wakamatwa,waonywa kuhusu usalama
Mweli:Wazee ni muhimu kwa maendeleo
Sijaja na miujiza,nipeni ushirikiano tuharakishe maendeleo :Kunenge