Na Joyce Kasiki, Geita
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameitaka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuongeza usimamizi wa matumizi ya kemikali katika migodi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya na usalama wa nguvu kazi inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji.
Aidha, amesema matumizi ya kemikali katika uzalishaji wa dhahabu ni sehemu muhimu ya shughuli za uchimbaji, hivyo usimamizi wake unapaswa kupewa kipaumbele ili kuzuia madhara kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Sangu metoa kauli hiyo leo, Septemba 24, 2026, katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, aliposhiriki Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini.
Amesema zebaki ni miongoni mwa kemikali zinazotumika katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wachimbaji wanapata elimu ya kutosha kuhusu matumizi salama pamoja na vifaa stahiki vya kujikinga.
Kwa mujibu wa Sangu, elimu kwa wachimbaji wadogo inapaswa kufikishwa moja kwa moja maeneo wanakofanyia shughuli zao, badala ya kusubiri wafike katika ofisi za mamlaka husika.
“Wachimbaji wadogo wanahitaji zaidi ya leseni. Wanahitaji maarifa yatakayowawezesha kufanya kazi zao bila kuhatarisha maisha na afya zao,” amesema Sangu.
Amesema ushirikiano kati ya Sekta ya Madini na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali unapaswa kuimarishwa kutokana na nafasi ya kemikali katika shughuli za uzalishaji madini.
Aidha, ameitaka Ofisi hiyo kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wachimbaji wadogo, hususan vijana wanaoingia katika sekta ya madini, ili waweze kutambua madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya kemikali.
Sangu amesema juhudi hizo zinaendana na Nguzo ya Pili ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii.
Amesema kulinda afya ya vijana wanaoshiriki katika uzalishaji ni sehemu ya kujenga nguvu kazi yenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa kwa muda mrefu.

More Stories
Miradi ya kusambaza umeme vitongojini kukamilika ifikapo 2030
Visima vya umwagiliaji vyawakomboa wakulima wadogo
Sangu atoa wito kwa waajiri kujisajili WCF