September 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madereva guta 72 wakamatwa,waonywa kuhusu usalama

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata madereva 72 wa pikipiki za mizigo za magurudumu matatu aina ya guta, pamoja na vyombo vyao na mizigo, baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, hususani katika upakiaji wa mizigo.

Baada ya kuwakamata,jeshi hilo liliwapa elimu madereva hao kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama wakati wa kusafirisha mizigo, huku likiwaonya kuacha tabia ya kupakia mizigo kwa namna inayohatarisha usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza Septemba 23,2026 na vyombo vya habari mara baada ya kutoa elimu kwa madereva hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa amesema,jeshi hilo limekuwa likipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya madereva wa pikipiki za magurudumu matatu wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, hususani katika upakiaji wa mizigo.

Amesema,taarifa hizo zilifanyiwa kazi na Jeshi la Polisi na kubaini kuwa vitendo hivyo vinaendelea, ambapo katika hatua hiyo madereva 72 pamoja na vyombo vyao na mizigo walikamatwa na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama wakati wa kusafirisha mizigo.

DCP.Mutafungwa amesema,upakiaji huo ni hatari kwa kuwa vyombo hivyo hutumia barabara zinazotumiwa na makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo watembea kwa miguu, wanafunzi na madereva wa magari, huku akisisitiza kuwa kubeba mizigo inayozidi ukubwa wa chombo kunaweza kusababisha ajali na madhara mengine.

Amesema,kumekuwa na matukio ya ajali yanayohusishwa na upakiaji wa mizigo kwa namna hatarishi, akitoa mfano wa chombo cha magurudumu matatu kilichokuwa kimebeba miringoti iliyotoka nje ya upana wa chombo na kugonga gari lililokuwa likitokea mbele, hali iliyosababisha dereva kupoteza maisha.

Hata hivyo amesema,jeshi hilo limeamua kutoa elimu kwa madereva hao badala ya kuchukua hatua za kisheria pekee, huku akimuelekeza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP.Sunday Ibrahim, kuandaa kikao cha elimu kwa madereva hao kitakachofanyika siku ya Ijumaa, ili kuwasaidia kuelewa madhara ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani.

Hivyo, amewataka madereva hao kutambua kuwa barabara ni ya watumiaji wote na kwamba wanapaswa kuzingatia usalama wa wengine wanapofanya shughuli zao za usafirishaji, pamoja na kuwa makini kwa kuhakikisha wanatazama pande zote na kutoa nafasi kwa watumiaji wengine wa barabara kabla ya kuendelea na safari.

“Watumiaji wa barabara si nyie pekee. Kila mmoja ana haki ya kutumia barabara, hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wa wengine kwa kutazama kushoto na kulia kabla ya kukata kona au kuingia kwenye barabara nyingine,” amesema.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, hatua ya kutoa elimu kwa madereva hao inalenga kuwajengea uelewa kuhusu matumizi salama ya barabara na umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu wakati wa usafirishaji wa mizigo.