Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Mbarali
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imesisitiza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika maendeleo ya jamii, huku ikiendelea kuweka mkazo katika upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii hususani afya.
Hayo yamesemwa Septemba 23,2026 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli,katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kata ya Kongolo wilayani humo.

Mweli amesema,katika kutekeleza azma hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ina hospitali mbili, ambazo ni Hospitali ya Wilaya na Chimala Mission pamoja na zahanati 64 na vituo vya afya 11 vinavyotoa huduma kwa wananchi, wakiwemo wazee.
Amesema,huduma hizo zinalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya kwa wakati, huku wazee wakiwa miongoni mwa makundi yanayohitaji kupewa kipaumbele kutokana na mahitaji yao ya kiafya.
Kuhusu ushirikishwaji wa wazee katika vikao vya maamuzi, Mweli alisema, halmashauri imeanza kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Ushauri la Wazee na taarifa zaidi zitatolewa baada ya hatua hizo kukamilika.
Pia amesema,ushirikishwaji wa wazee ni muhimu kutokana na uzoefu na busara walizonazo, ambao unaweza kusaidia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Hezron Kapwela,amewataka vijana kutumia nguvu na uwezo walionao kujijengea maisha bora mapema, ikiwemo kujenga nyumba na kujiandaa kwa maisha ya uzeeni.
Kapwela amesema,vijana wanapaswa kuanza maandalizi ya maisha ya baadaye wakiwa bado wana nguvu za kufanya kazi, ili kupunguza utegemezi kwa watoto wao wanapofikia uzee.
“Tunawaasa vijana jengeni nyumba mkiwa bado mna nguvu, msije mkawa kama wazee wanaolalamika sasa hivi kwamba watoto hawanijengei nyumba, wakati yeye alianza kuwa na nguvu na nguvu zimepotea sasa anaanza kutishia kutoa laana kwa watoto, hiyo laana hata Mungu haipokei,”amesema Kapwela.

Akisoma risala katika maadhimisho hayo, Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee la Halmashauri hiyo, Michael Sanga,ameiomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wazee, ikiwemo kujenga na kukamilisha vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo havijakamilika.
Sanga amesema,kuboreshwa kwa huduma hizo kutawasaidia wazee kupata huduma muhimu kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa kundi hilo kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kuanzia ngazi ya kata hadi halmashauri.
“Tunaomba wazee washirikishwe katika vikao vya maamuzi, kuanzia Kamati za Maendeleo za Kata hadi vikao vya Halmashauri, ili tupate fursa ya kutoa mawazo na kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii,”amesema Sanga.


More Stories
Watanzania waonywa matumizi holela ya dawa
Madereva guta 72 wakamatwa,waonywa kuhusu usalama
Sijaja na miujiza,nipeni ushirikiano tuharakishe maendeleo :Kunenge