WATANZANIA wamehimizwa kuendelea kudumisha maadili mema na kuwa mfano bora katika jamii ili kujenga Taifa lenye amani, umoja na mshikamano.
Wito huo umetolewa wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Maadili uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni.
Mdahalo huo, umelenga kuhamasisha na kuchochea uendelezaji wa maadili mema miongoni mwa Watanzania.
Watoa mada katika mdahalo huo wamesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kutambua kuwa ni sehemu ya jamii na hivyo anapaswa kuwa “kioo” bora kinachoonesha mfano mwema kwa wengine.
Wameeleza kuwa matendo ya mtu yanaweza kuwa chachu ya kuigwa na jamii, hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha anasimamia maadili mema katika maisha yake ya kila siku.
Aidha, imesisitizwa kuwa maadili ni msingi wa utu, umoja na mshikamano wa kitaifa, hivyo yana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye kuheshimiana na taifa lenye amani na maendeleo.
Watanzania pia wamehimizwa kuwa mfano bora kwa watoto na jamii kwa ujumla, kuipenda Tanzania kwa vitendo, kuheshimu utu wa wengine na kushiriki katika kujenga taifa lenye amani, umoja na mshikamano.
Watoa mada wamesisitiza kuwa maadili mema si suala la mtu mmoja pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania, kwa kuwa ndiyo yanayounda na kuimarisha utambulisho wa Taifa.
Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linaendelea kuwakutanisha wadau mbalimbali katika kuenzi, kukuza na kuendeleza utamaduni wa Tanzania pamoja na kuhamasisha jamii kuthamini misingi inayojenga Taifa.

More Stories
Elimu ulinzi shirikishi yapunguza mauaji Kwimba
AIRTEL FURSA LAB yarudi kwa sura mpya
Mshikemshike: Ufugaji wabadili maisha Shinyanga