Na Mwandishi wetu,Timesmajira
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 11, akiwemo Timothy Eshemo maarufu kwa jina la Jack, kwa tuhuma za kuiba miundombinu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Taarifa hiyo ilitolewa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
SACP Muliro amesema baadhi ya watuhumiwa hao wanadaiwa kujihusisha na kupanga uhalifu, kuiba pamoja na kununua miundombinu hiyo kwa lengo la kufanya biashara.
Amesema miundombinu inayodaiwa kuibwa ni pamoja na nyaya za shaba (copper cables), ambazo zimekuwa zikisababisha kukatika au kuathiriwa kwa huduma za mawasiliano katika taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi.“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linalaani hujuma hizi na litawashughulikia wale wote wanaohusika kupanga na kuiba miundombinu hiyo,” amesema SACP Muliro.
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, zoezi la kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa hao limefanyika kuanzia Juni hadi Agosti 2026 kwa kushirikiana na Kitengo cha Usalama cha TTCL.

Amesema baadhi ya watuhumiwa walitumia mbinu ya kujifanya wafanyakazi wa TTCL ili kupata nafasi ya kufikia miundombinu hiyo na kuiba nyaya zenye shaba.
“Uhalifu umefanyika katika maeneo ya Kinondoni, Upanga na Mikocheni, ambapo watuhumiwa hao walikuwa wanaongozwa na mtu anayejulikana kwa jina la Timothy Eshemo maarufu kama ‘Jack’,” amesema SACP Muliro
Jeshi la Polisi limeendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao mzima wa watu wanaodaiwa kuhusika na wizi huo pamoja na hatua nyingine za kisheria dhidi ya watuhumiwa.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam lilisema kuwa hali ya usalama inaendelea vizuri huku likitoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili kukomesha vitendo vya uhalifu.

More Stories
Watanzania wahimizwa kudumisha maadili
Elimu ulinzi shirikishi yapunguza mauaji Kwimba
AIRTEL FURSA LAB yarudi kwa sura mpya