August 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EAC yaweka mkazo kubadili ahadi za elimu

Na Mwandishi wetu,Nairobi

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeelekeza nguvu katika kubadili ahadi na mipango ya elimu kuwa matokeo yanayopimika,huku takribani wajumbe 600 kutoka nchi nane wanachama wakitarajiwa kukutana jijini Nairobi kujadili mustakabali wa elimu katika ukanda huo.

Taarifa iliyotolea kwa vyombo vya habari jana nchini Nairobu imesema mkutano huo ni wa pili wa EAC wa Elimu wa Kikanda unaofanyika kuanzia Agosti 25 hadi 28,mwaka huu.

Imesema mkutano huo unafanyika ikiwa nchi za Afrika Mashariki zikiendelea kukabiliwa na changamoto za pengo la ujifunzaji, ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa elimu na uhaba wa walimu na rasilimali.

Mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa kwanza uliofanyika Arusha, Tanzania, mwaka 2024, na kuweka mikakati itakayosaidia kuhakikisha ahadi hizo zinageuka kuwa mabadiliko halisi kwa wanafunzi na jamii.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkutano huo, licha ya nchi wanachama kupiga hatua katika kuongeza upatikanaji wa elimu na kufanya mageuzi mbalimbali,bado watoto wanaoishi vijijini na katika jamii zilizotengwa wanaendelea kukabiliwa na changamoto za kupata elimu bora.

Wanafunzi wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi pia wanatajwa kuwa miongoni mwa wanaohitaji kupewa kipaumbele katika juhudi za kujenga mfumo wa elimu unaozingatia usawa na ujumuishi.

Aidha, changamoto ya ubora wa elimu bado ni kubwa, huku uhaba wa walimu, upungufu wa rasilimali na udhaifu wa mpito kutoka ngazi moja ya elimu kwenda nyingine ukiendelea kuwanyima baadhi ya vijana njia nzuri ya kuendelea na masomo au kuingia katika ajira.

Mkutano huo umeweka pia mkazo katika pengo linalozidi kujitokeza kati ya elimu inayotolewa na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa hali hiyo, washiriki watajadili namna ya kuimarisha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), pamoja na kujenga uhusiano mkubwa kati ya taasisi za elimu na sekta binafsi ili wahitimu wawe na ujuzi unaohitajika katika ajira, ujasiriamali na uchumi wa kisasa.

Ukuaji wa idadi ya vijana katika Afrika Mashariki umeongeza umuhimu wa suala hilo, kutokana na ongezeko la vijana wanaohitaji elimu, ujuzi na fursa za kiuchumi.

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu “Transforming Education in East Africa: From Commitments to Impact, Fostering Resilience and Future-Ready Systems for Sustainable Development,” inayosisitiza mabadiliko kutoka kwenye ahadi kwenda kwenye matokeo.

Katika mkutano huo, wajumbe wanatarajiwa kujadili namna ya kuimarisha elimu ya awali na ujifunzaji wa msingi, kuongeza uwezo wa walimu na kupanua elimu jumuishi.

Pia wataangalia namna ya kujenga njia bora zinazowaunganisha wanafunzi kutoka elimu na mafunzo hadi kwenye ajira zenye staha.

Teknolojia nayo inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya majadiliano, hasa kutokana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali na kuibuka kwa teknolojia mpya, ikiwemo akili mnemba.

Kwa upande mwingine, mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali za nchi wanachama, vyuo na taasisi za elimu, taasisi za TVET, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo.

Ushirikiano huo unalenga kuboresha ubora na umuhimu wa elimu ya juu, kuwezesha ulinganifu wa mifumo ya elimu na kujenga nguvu kazi yenye ujuzi inayoweza kutumia fursa zinazopatikana ndani ya soko la Afrika Mashariki.

Mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo ya sera na hatua za utekelezaji zitakazosaidia nchi wanachama kufuatilia maendeleo katika maeneo ya upatikanaji wa elimu, usawa, ubora na matokeo ya ujifunzaji.