August 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkenda aitaka EAC kuongeza uwekezaji Sekta ya Elimu

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda, amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya elimu, mafunzo ya walimu na vifaa bora vya kujifunzia ili kuboresha ubora wa elimu katika ukanda huo.

Prof. Mkenda ametoa wito huo jana katika Mkutano wa Pili wa Kikanda wa EAC kuhusu Elimu unaofanyika Nairobi nchini Kenya,ulioanza Agosti 25 hadi 28, 2026, ukiwakutanisha mawaziri wa elimu, watunga sera, walimu, watafiti na washirika wa maendeleo.

Amesema kuboresha upatikanaji na ubora wa elimu ya msingi na sekondari kunahitaji uwekezaji endelevu katika shule, kuwaandaa walimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata vifaa bora vya kujifunzia.

Mkutano huo, wenye kaulimbiu “Kubadilisha Elimu Afrika Mashariki,Kutoka Ahadi hadi Matokeo, Kukuza Mifumo Imara na Tayari kwa Mustakabali kwa Maendeleo Endelevu,” unalenga kuhamasisha utekelezaji wa hatua za pamoja zitakazoboresha matokeo ya elimu katika ukanda huo.

Prof. Mkenda amesema uwekezaji wa kitaifa unapaswa kwenda sambamba na ushirikiano wa kikanda, hususan katika kuoanisha mifumo ya elimu, mitaala, viwango na sifa za kitaaluma ili kurahisisha uhamaji wa wanafunzi na wataalamu ndani ya Afrika Mashariki.

Awali akizungumza wakati wa kufungua Mkutano huo,Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Kijamii na Kisiasa EAC, Ariik Malueth,amesema Jumuiya hiyo imepiga hatua katika kuandaa mifumo ya kuoanisha elimu na maendeleo ya ujuzi, lakini sasa kinachohitajika ni utekelezaji wenye matokeo.

Malueth amesema elimu na maendeleo ya ujuzi ni msingi wa ujumuishaji wa Afrika Mashariki, huku akitaja mipango ya kuimarisha mifumo ya elimu ya msingi na Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Stadi (TVET).

Amesema EAC pia inalenga kuoanisha mitaala ya TVET, utambuzi wa vyeti, sifa za kitaaluma na mifumo ya uhakikisho wa ubora ili vijana waweze kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la kikanda.

Aidha, amesema elimu ya kidijitali, mafunzo ya walimu na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika mageuzi ya elimu ya Afrika Mashariki.