Na Mwandishi Wetu,Dodoma
TUME ya Taifa ya Umwagiliaji imekutana na Tume ya Taifa ya Mipango,Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,kwa lengo la kujadili namna bora ya kuoanisha mipango, miradi na utekelezaji wa shughuli zake ili kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mtendaji wa Menejimenti ya Utendaji na Tathmini kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Sosthenes Kewe, amesema ni umuhimu kwa miradi ya Umwagiliaji kuwa na matokeo yanayoonekana kwa jamii pamoja na kuzingatia vipaumbele vya taifa.

Ameeleza kuwa ni muhimu taasisi zote kuhakikisha miradi yao inaendana na mipango ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu, huku ikionesha uwajibikaji na kuinua uchumi wa wananchi
“Tunapaswa kuzingatia miradi yenye matokeo zaidi kwa jamii, inayotanguliza vipaumbele vya taifa na kuonesha matokeo halisi yanayoboresha maisha ya Watanzania,” amesisitiza.
Amesema, sekta ya Umwagiliaji ni kubwa katika kufikia malengo ya maendeleo ya kitaifa hivyo ni muhimu kazi zinazotekelezwa na NIRC na uwekezaji unaoenelea uendane na mipango ya nchi kwa kuzingatia malengo ya kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu na uratibu madhubuti kati ya taasisi hizo ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
“Ni muhimu tuanze pamoja ili kuhakikisha yale tunayoyafanya yanaendana na mipango ya nchi. Pale tunapokwenda vizuri tuendelee, lakini pia turekebishane mapema ili kuepuka upotevu wa rasilimali za Serikali na kuongeza ufanisi katika utekelezaji,” amesema Mndolwa.

Kikao hicho pia kililenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ikiwemo uingizaji wa miradi kwenye mifumo rasmi ya ufuatiliaji na tathmini, kuongeza ubora wa taarifa za utekelezaji na kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kuvutia uwekezaji na kuonesha mchango wa sekta ya Umwagiliaji katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa ujumla, majadiliano hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zake, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi zaidi ili kuleta matokeo chanya na ya kudumu kwa jamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi.


More Stories
Mkenda aitaka EAC kuongeza uwekezaji Sekta ya Elimu
EAC yaweka mkazo kubadili ahadi za elimu
Polisi yawashikilia watu 11 wizi wa miundombinu ya TTCL