Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Kwimba
IMEELEZWA kuwa elimu ya ulinzi shirikishi inayotolewa na Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Polisi Jamii imetajwa kupunguza vitendo vya mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina na mila potofu wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Akizungumza Agosti 25,2026kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza Ng’wilabuzu Ludigija alisema,elimu hiyo na ushirikiano kati ya wananchi, Jeshi la Polisi na vikundi vya Sungusungu,imesaidia wilaya hiyo kukaa kati ya miezi nane hadi mwaka bila kushuhudia mauaji yanayoambatana na mila potofu.
“Hii yote inatokana na wananchi kulipokea Jeshi la Polisi na maofisa hawa kufanya kazi nzuri ya kuelimisha jamii.Pia ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Sungusungu imesaidia kuimarika kwa hali ya usalama wilayani humo,”amesema Ludigija.

Hata hivyo amesema,Serikali itaendelea kuliunga mkono Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri inayofanywa katika kuimarisha usalama na uhusiano na wananchi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa amesema,falsafa ya Polisi Jamii imesaidia kuimarika kwa utoaji wa taarifa za uhalifu na kupungua kwa baadhi ya makosa, yakiwemo mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina.
Amesema,Mkoa wa Mwanza umeweka Wakaguzi na Polisi Kata katika kata zote 191 ili kusogeza huduma za ulinzi karibu na wananchi.Hivyo alisisitiza kuwa vikundi vya Sungusungu vinapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuzingatia utu na haki za binadamu, huku akivitaka kuepuka kujichukulia sheria mikononi.
kwa upande wake, Mtemi wa Sungusungu Kanda ya Ziwa, Shimbi Morgani amesema,Polisi Jamii imefanikiwa kubadilisha kwa kiwango kikubwa uhusiano uliokuwepo kati ya wananchi wa Mwanza na Jeshi la Polisi.
“Zamani baadhi ya wananchi walikuwa wakiwaogopa polisi na kuwakimbia kila mmoja ukimsogelea,sasa hivi anamwona polisi kama ndugu yake. Tunaomba Jeshi la Polisi liendelee kuimarisha uhusiano na wananchi,”amesema Morgan.



More Stories
AIRTEL FURSA LAB yarudi kwa sura mpya
Kikundi cha Mshikemshike cha badilisha maisha kwa Ufugaji wa Kondoo Shinyanga
NMB yaibuka Superbrand Afrika Mashariki 2026-2028