August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kuhamasisha vijana kuchapa kazi

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online- Ileje.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe,Osiwelo Chomo, amewataka Watendaji wa Kata, Madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo kutumia uelewa na taaluma zao kuhamasisha jamii, hususani vijana, kujenga utamaduni wa kufanya kazi na kujikita katika shughuli za uzalishaji.

Chomo ametoa kauli hiyo wakati akifunga kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Ileje kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri  hiyo, kilicholenga kupitia na kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/26.

Amesema vijana wanapaswa kuhamasishwa kutumia muda wao katika shughuli zenye tija badala ya kujihusisha na mambo yasiyokuwa na mchango katika maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla.

“Tunapaswa kuwahamasisha vijana kufanya kazi kwa bidii, kwa sababu kupitia uzalishaji ndipo wataweza kujiletea maendeleo yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,”amesema Chomo.

Sanjari na hayo,Chomo amevihasa vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki,sheria na taratibu ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wananchi.

Amesema katika operesheni na misako inayofanyika kwenye maeneo mbalimbali, ni muhimu watendaji wa vitongoji,vijiji na kata kushirikishwa ili kuimarisha mawasiliano,uwazi na ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.

Awali, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje Hassan Lyamba amesema,chama hicho kimeridhishwa na utendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali hususani utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha zinazotolewa na Serikali.

Lyamba amewapongeza wataalamu wa halmashauri kwa usimamizi mzuri wa fedha na juhudi za ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambapo alisema halmashauri hiyo imefikia asilimia 107 ya lengo la makusanyo.

Hata hivyo,amewataka wataalamu hao kuongeza ubunifu na kasi katika ukusanyaji wa mapato ili kuendelea kuimarisha uwezo wa halmashauri katika kutoa huduma na kutekeleza miradi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje, Abdala Mayomba, akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, amewataka madiwani na watendaji wa kata kuhakikisha wanasikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Mayomba pia amesisitiza umuhimu wa kulinda amani, akieleza kuwa utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo na kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuudumisha.