August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha Ubia chakutana na Wanahabari kutekeleza agizo la Rais

Na.Mwandishi weti,Timesmajira

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, ameanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukutana na waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.


Kikao hicho cha kimkakati kilichofanyika Jumanne, Agosti 4, 2026, katika ofisi za PPPC jijini Dar es Salaam.

Kafulila amekutana na waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii siku moja baada ya Rais Samia kutangaza, wakati wa uzinduzi wa nyenzo za utekelezaji wa Dira 2050 uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, kuwa nchi sasa inaingia katika hatua ya utekelezaji wa vitendo na kwamba muda wa maneno umekwisha.

Katika kikao hicho, Kafulila amesema hatua ya kukutana na wamiliki na waandishi wa majukwaa ya kidijitali inalenga kutekeleza agizo la moja kwa moja la Rais Samia, aliyezitaka taasisi za umma kutoa elimu kwa wananchi ili wafahamu fursa zilizopo na kudhibiti makundi yanayoweza kujitokeza kupotosha malengo ya Dira ya Taifa.

“Ili kufikia lengo la kujenga uchumi utakaokuwa na uzalishaji wa bidhaa na huduma wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja katika miaka 25 ijayo (2026–2050), lazima kuwe na mshikamano wa dhati kati ya serikali, sekta binafsi, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla,” amesema Kafulila katika kikao hicho.

Rais Samia amebainisha majukumu ya sekta binafsi, akisema kuwa imekabidhiwa ‘funguo’ za mustakabali wa nchi na inatarajiwa kuendesha asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira 2050 katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

“Sekta binafsi imepewa takribani asilimia 70 katika utekelezaji wa Dira hii kwa miaka 25 ijayo,” amesema.

“Kwa upande wetu kama serikali, tutaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje,” ameongeza Rais Samia.


Nyenzo nne zilizozinduliwa kusaidia utekelezaji wa Dira 2050 ni: Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV), Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini, pamoja na Mkakati wa Mawasiliano.