August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahamasisha uwekezaji kupitia TBA

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

SERIKALI imewahimiza wadau wa sekta binafsi, kampuni na wananchi mmoja mmoja kutumia fursa za uwekezaji zinazotolewa kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza tija kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, Agosti 5, 2026, alipotembelea banda la TBA katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma.

Dkt. Msonde amesema Serikali imeboresha sheria na kanuni zinazosimamia TBA ili kuipa uwezo mkubwa wa kushirikiana na sekta binafsi katika kupata rasilimali za kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa utekelezaji wa miradi na kuongeza kasi ya maendeleo kupitia ushiriki wa wawekezaji binafsi.

Aidha, amesema TBA ina wataalamu wenye uwezo wa kubuni majengo ya kisasa pamoja na mazingira bora yanayoweza kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Msonde, amesema maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yameandaliwa kwa kuzingatia vigezo vinavyohitajika, hivyo kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali inatarajia sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya pato linalolengwa, jambo linaloifanya hii kuwa fursa muhimu kwa wawekezaji kutumia huduma na miradi inayoratibiwa na TBA.

Dkt. Msonde amesema tayari Serikali imeanza kupokea mwitikio kutoka kwa wawekezaji na kutoa wito kwa wananchi, kampuni na wadau wengine kujitokeza kwa wingi kuwekeza kupitia TBA ili kujiongezea kipato na kuongeza mapato ya Serikali kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.