August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Kabudi aitaka Kilosa iendelee kulinda amani

Na Mwandishi Wetu, Kilosa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), amewataka wananchi wa Jimbo la Kilosa kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano, huku wakiepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa jamii na kudhoofisha shughuli za uzalishaji.

Kabudi alitoa rai hiyo,Agosti 5, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Magomeni, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Akizungumza na wananchi, Waziri Kabudi amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha sekta ya mifugo kwa kuwawezesha wafugaji kuanzisha malisho ya kisasa, badala ya kutegemea mfumo wa kuchunga mifugo kihamahama.

Amesema tayari eneo la Madoto limetengwa kwa ajili ya shamba la majaribio la malisho, hatua inayolenga kuhamasisha ufugaji wa kisasa wenye tija na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

“Tunataka wafugaji watoke kwenye utaratibu wa kuchunga na waingie katika mfumo wa kufuga kwa tija. Hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha amani katika jamii,”amesema Prof. Kabudi.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali imekusudia kuufanya ukanda unaopitiwa na Reli ya Kisasa (SGR) kuwa kitovu cha uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya biashara.

“Tunataka ukanda huu unaopitiwa na SGR, kuanzia Lumuma–Kidete hadi Mkata, uwe eneo la kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya biashara ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi,”amesema.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Serikali inaendelea na hatua za kutangaza mabonde ya Kisaki, Manyenyere, Mabana na Mbigiri kuwa maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya mbogamboga.

Amesisitiza kuwa mabonde hayo yana umuhimu mkubwa si kwa wananchi wa Kilosa pekee, bali kwa maendeleo ya taifa, hivyo yanapaswa kulindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Baada ya maeneo haya kutangazwa rasmi, kila mmoja anatakiwa kutambua kuwa ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa taifa. Atakayeyaharibu au kuyatumia kinyume cha utaratibu atakuwa amegusa maslahi mapana ya nchi,”amesisitiza.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Magomeni, Dkt. Sudi Salum,amesema migogoro kati ya wakulima na wafugaji bado ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kudumisha amani na kuongeza uzalishaji.

Amesema baadhi ya vitendo vya kihalifu, ikiwemo kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwa makusudi, vimekuwa vikichochea migogoro isiyo ya lazima.

“Hatusemi kwamba wakulima na wafugaji hawahitajiani. Wanahitajiana, lakini ni lazima kujenga misingi ya kuheshimiana, kufuata sheria na kuishi kwa maelewano,”amesema Dkt. Sudi.

Naye mwananchi wa Kata ya Magomeni, Tausi Ally, aliiomba Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi shirikishi ili kudhibiti vitendo vya uhalifu, ikiwemo unyang’anyi wa mali na mashambulizi ya kimwili, vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri maendeleo ya Jimbo la Kilosa.

Amesema kuimarishwa kwa ulinzi na usalama kutasaidia wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji katika mazingira ya amani na utulivu.