August 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amewataka watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuongeza bidii, uwajibikaji na kuachana na utendaji wa kazi kwa mazoea ili kuhakikisha majukumu ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Makamu wa Rais ametoa wito huo leo, alipofanya ziara yake ya kwanza katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), iliyopo Mtumba, jijini Dodoma, ambako alipokelewa na wafanyakazi pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo.

Amesisitiza umuhimu wa watumishi kubadili mitazamo na namna ya kufanya kazi, akitaka kila mmoja kuwa mbunifu na kuweka mipango inayolenga kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amewasihi watumishi kutumia nafasi zao kutoa huduma yenye thamani kwa watanzania na kutambua dhamana waliyonayo katika kuwahudumia wananchi. Pia amewataka kubadili mitazamo na namna ya kufikiri, kuwa wabunifu na kuhakikisha mipango inayowekwa inaleta tija na matokeo chanya katika shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

Halikadhalika, amewataka kuongeza jitihada katika kudumisha Muungano kwa kuwa na mipango endelevu inayolenga kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kutoa elimu ya fursa zilizopo katika Muungano.

Amewasihi Viongozi na Watumishi wa Wizara hiyo, kuwa na mipango endelevu katika utekelezaji wa ajenda ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa kutumia vema kampeni za upandaji miti, usafi wa majiji na miji kwa kuweka nyenzo zitakazosaidia kufanya hali hiyo kuwa endelevu. Vile vile amesisitiza umuhimu wa kuwa na Mpango maalum utakao saidia wananchi kuhama katika shughuli za kila siku zinazoharibu mazingira.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amempongeza Makamu wa Rais kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika nafasi hiyo na kumhakikishia ushirikiano katika kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusu Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akiwasilisha taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na idara mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi, amesema wizara hiyo ina Idara nne, Vitengo nane na Taasisi mbili zinazotekeleza majukumu mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika masuala ya Muungano na Mazingira.