August 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Serbia kuongeza fursa za biashara

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Jamhuri ya Serbia, hususan katika biashara na uwekezaji, kilimo, utalii na Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo tarehe 31 Agosti 2026 jijini Belgrade, nchini Serbia, alipokutana na Rais wa Jamhuri ya Serbia, Aleksandar Vučić, katika Kasri la Serbia.

Amesema Tanzania na Serbia zina historia ndefu ya urafiki na ushirikiano, iliyojengwa katika misingi ya kuheshimiana na mshikamano, akibainisha kuwa uhusiano kati ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais Josip Broz Tito uliweka msingi muhimu wa mahusiano hayo.

Rais Dkt. Mwinyi amemfikishia Rais Vučić salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.

Aidha, ameupongeza uamuzi wa Serbia wa kufungua Ubalozi wa kudumu nchini Tanzania na kueleza kuwa Tanzania tayari imetenga eneo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi huo na makaazi ya Balozi.

Katika kukuza biashara na utalii, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Serbia na Tanzania, zitakazohudumia Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wake, Rais Aleksandar Vučić amesisitiza utayari wa Serbia kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania, akieleza kuwa Serikali yake inaendelea kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali ya kukuza uhusiano huo.

Halikadhalika, Rais Vučić ameunga mkono kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Serbia na Tanzania, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza biashara, utalii na mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Rais Dkt. Mwinyi yupo Belgrade kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Kumbukumbu ya Miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).