Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Yumna Mmanga Omar, ameitaka Serikali kuweka utaratibu madhubuti wa kufuatilia vijana wenye ulemavu waliopatiwa mafunzo ya ufundi, ili kubaini ni wangapi wamepata ajira au wameanzisha biashara endelevu na kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kujikwamua kiuchumi.
Yumna alitoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akiuliza swali la msingi na la nyongeza Bungeni kuhusu mikakati ya Serikali katika kulea na kuendeleza vipaji na ujuzi wa vijana wenye ulemavu, hususan katika kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika elimu na ajira.
Katika swali lake la msingi, Mbunge huyo aliitaka Serikali kueleza iwapo ina mkakati mahsusi wa kukuza vipaji na ujuzi wa vijana wenye ulemavu ili kuongeza fursa zao za ajira pamoja na ushiriki wao katika elimu.
Akijibu kwa niaba ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Jaffar Seif, alisema Serikali ina mikakati mbalimbali ya kitaifa inayolenga kukuza vipaji, ujuzi na kuwawezesha vijana wenye ulemavu kushiriki katika elimu, mafunzo ya ufundi, ajira na shughuli za kiuchumi.
Alisema mikakati hiyo inazingatia kwamba ulemavu haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu kutumia kipaji na uwezo wake katika kujiletea maendeleo.
Dkt. Seif alisema katika utekelezaji wa mikakati hiyo, jumla ya vijana 64 wenye ulemavu walijiunga na kumaliza mafunzo katika vyuo vitano vya ufundi stadi, ikiwamo VETA, katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, vijana hao waliwezeshwa kupata ujuzi katika fani mbalimbali, zikiwamo umeme, uashi, useremala, uchomeleaji, ushonaji wa nguo na viatu, ufugaji pamoja na ujenzi.
Aidha, alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kunufaika na fursa za kiuchumi, ikiwamo kutenga asilimia 10 ya zabuni za umma kwa makundi maalum.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2024/25, jumla ya vikundi 703 vilivyosajiliwa katika mfumo huo vimeweza kuingia katika mfumo wa ununuzi wa umma, hatua inayolenga kuhakikisha ujuzi wanaoupata unatumika katika kujiajiri na kuongeza kipato.
Dkt. Seif pia alisema Serikali imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa makundi maalum, ambapo asilimia mbili hutengwa kwa watu wenye ulemavu.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, jumla ya Sh bilioni 26.87 zimetolewa kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi.
Katika swali lake la nyongeza, Yumna aliitaka Serikali kueleza iwapo ina utaratibu wa kuwafuatilia vijana hao baada ya kumaliza mafunzo, pamoja na kutoa takwimu zinazoonyesha ni wangapi wamepata ajira, wamejiajiri au wameanzisha biashara endelevu.
Aliomba pia Serikali kuweka wazi matokeo halisi yaliyopatikana kutokana na uwekezaji huo, ili Bunge na wananchi waweze kutathmini manufaa ya programu hizo kwa vijana wenye ulemavu.
Akijibu swali hilo, Dkt. Seif alisema Serikali imeweka mfumo wa kupata taarifa kutoka Halmashauri zote nchini, huku wakurugenzi na watendaji wa maendeleo katika Halmashauri wakiendelea kuwafikia vijana wenye ulemavu kwa ajili ya kutoa elimu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali.
Alisema Serikali pia inahakikisha vijana hao wanapata fursa za mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri pamoja na kushiriki katika mfumo wa manunuzi ya umma.
Dkt. Seif alisema ongezeko la vikundi kutoka 45 mwanzoni hadi kufikia 703 sasa ni miongoni mwa viashiria vinavyoonyesha kuwa mfumo huo unaendelea kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwamo vijana, wanashirikishwa katika juhudi za kukuza uchumi wa Taifa na kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali.

More Stories
Serikali yahakikishia ajira wenye ulemavu
Watakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea
Tanzania,Serbia kuongeza fursa za biashara