Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Yumna Mmanga Omar, amehoji serikali kuhusu utaratibu unaotumika kuhakikisha wahitimu wenye ulemavu wanapata fursa za ajira na mafunzo yanayotokana na miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Yumna ametoa hoja hiyo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, akitaka kufahamu namna serikali inavyowaunganisha wahitimu wenye ulemavu na fursa zinazozalishwa na miradi hiyo.
Mbunge huyo amesema miradi mbalimbali ya kimkakati inaendelea kuzalisha fursa nyingi za ajira na mafunzo ya ujuzi, hivyo akauliza kama serikali ina utaratibu wa kuhakikisha wahitimu wenye ulemavu wanapata nafasi hizo na namna taarifa za fursa hizo zinavyowafikia.
Akijibu swali hilo, Waziri Sangu amesema serikali imekuwa ikitambua umuhimu wa kuwahusisha watu wenye ulemavu katika fursa za ajira zinazozalishwa na miradi ya kimkakati na imekuwa ikifanya ukaguzi kuhakikisha waajiri wanazingatia matakwa ya sheria.
Amesema kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, serikali imekuwa ikifanya ukaguzi mbalimbali ili kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, inayowataka waajiri kutenga sehemu ya nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu.
“Serikali itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha watu wenye ulemavu hawabaki kuwa wadau muhimu tu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, bali pia wanapata fursa za ajira,” amesema Waziri Sangu.
Katika swali la msingi lililoulizwa na Yumna Mmanga Omar kwa niaba ya Mbunge wa Viti Maalum, Asha Feruzi, Waziri Sangu amesema serikali imekuwa ikitumia miradi mikubwa ya kimkakati kuwaunganisha Watanzania kutoka makundi mbalimbali na fursa za ajira pamoja na kuwapatia wahitimu uzoefu wa kazi.
Amesema takribani ajira 35,000 zimezalishwa katika ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), huku ajira 10,000 zikitokana na mradi wa bomba la mafuta, ajira 10,000 katika ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na ajira 1,500 katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Aidha, amesema ajira 1,500 zimezalishwa katika ujenzi wa Daraja la Kigongo pamoja na fursa nyingine zinazotokana na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Sangu amesema hatua nyingine inayochukuliwa na serikali ni kuimarisha programu za mafunzo kwa vitendo, ikiwemo mafunzo ya muda kwa wahitimu, ili kuwawezesha kupata uzoefu unaoendana na mahitaji ya waajiri.
Kwa mujibu wa Waziri, hadi Aprili 2026, jumla ya wahitimu 20,000 walikuwa wamepatiwa mafunzo hayo huku akisema kuwa serikali imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu wa mwaka 2017, unaohusu utekelezaji wa mafunzo hayo katika sekta ya umma na binafsi.
Pia, amesema serikali inaendelea kujenga uwezo wa vijana na wafanyakazi katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya kitaaluma na ujuzi, ambapo hadi Aprili 2026 jumla ya Watanzania 168,000 walikuwa wamenufaika na programu hiyo.
Hatua hizo, kwa mujibu wa Waziri Sangu, zinalenga kuongeza uwezekano wa wahitimu na Watanzania wengine kupata ujuzi, uzoefu na fursa za ajira zinazotokana na miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.

More Stories
Serikali iweke mikakati ya ajira kwa wenye ulemavu
Watakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea
Tanzania,Serbia kuongeza fursa za biashara