August 31, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaongeza ulinzi watoto dhidi ya ukatili mtandaoni

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

SERIKALI imeeleza kuwa imechukua hatua mbalimbali kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, unyanyasaji na madhara ya kidijitali yanayotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii, ikiwemo kuwafikia zaidi ya watoto milioni 1.8 kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Marypriscar Mahundi, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Licy Kombani, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukatili mtandaoni kutokana na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii.

Akijibu swali hilo, Mhandisi Mahundi amesema Serikali inaendelea kuhakikisha watoto wananufaika na teknolojia huku wakilindwa dhidi ya ukatili, unyanyasaji, unyonyaji na madhara mengine ya kidijitali.

Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, iliyofanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kampeni hiyo imelenga kutoa elimu kwa watoto, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhusu matumizi salama na yenye uwajibikaji ya teknolojia, pamoja na kulinda haki za watoto wanapotumia mitandao na mifumo ya kidijitali.

Amesema kupitia kampeni hiyo, jumla ya watoto 1,811,212 wamefikiwa na elimu kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni.

Aidha, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, ambayo ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu pamoja na kusaidia kuweka mikakati na afua madhubuti za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili na madhara yanayoweza kuwakabili watoto wanapotumia mifumo ya kidijitali.

Katika swali lake la nyongeza, Kombani alihoji kuhusu taratibu zinazotumiwa na Serikali kuhakikisha teknolojia wanayotumia watoto, ikiwemo simu na tablet, haiwi chanzo cha wao kukutana na maudhui hatarishi au kushiriki katika vitendo vya ukatili mtandaoni.
Amesema kumekuwa na ongezeko la matumizi ya vifaa vya kielektroniki kwa watoto, hali inayohitaji usimamizi wa karibu ili kuhakikisha teknolojia inatumika kwa manufaa yao na si kuwa chanzo cha madhara.

Akijibu swali hilo la nyongeza, Mhandisi Mahundi amesema Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni inahusisha wadau mbalimbali, wakiwemo kutoka Wizara inayohusika na masuala ya Habari na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Amesema Serikali inaendelea kujadili kwa pamoja namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi makubwa ya intaneti, huku ikihakikisha watoto wanabaki salama wanapotumia teknolojia.

Naibu Waziri amesema si rahisi kuwaondoa watoto kwenye matumizi ya teknolojia kutokana na ukweli kwamba dunia ya sasa inawahitaji kuwa na ujuzi wa kidijitali, na mara nyingi watoto huweza kuifahamu teknolojia kwa kiwango kikubwa kuliko wazazi wao.

Hata hivyo, amewataka wazazi na walezi kuchukua jukumu la karibu katika kufuatilia matumizi ya vifaa vya kielektroniki vya watoto wao, akisisitiza kuwa mzazi anayemnunulia mtoto simu au tablet anapaswa pia kufahamu programu na maudhui anayoyatumia mtoto huyo.

Amesema usimamizi huo ni muhimu kwa watoto wa rika mbalimbali ili kuwasaidia kuepuka maudhui yanayoweza kuwadhuru au kuwaingiza katika vitendo ambavyo vinaweza kuwa na madhara kwa maisha yao ya baadaye.

Mhandisi Mahundi amesisitiza kuwa malezi chanya ni jukumu la jamii nzima, huku akiwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao, kufuatilia wanachofanya mtandaoni na kuzungumza nao kuhusu matumizi salama na yenye uwajibikaji ya teknolojia.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wazazi, walezi, jamii na wadau wa teknolojia ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya kidijitali hayaendi sambamba na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni.