December 6, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wasiosikia waelimishwa kuhusu Covid-19

Na Esther Macha, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa Kanda ya Mbeya imetoa elimu ya kupambana maambukizi ya virusi vya Corona kwa  watu wenye  ulemavu wa kusikia .

Akizungumza na majira juzi ofisini kwake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dkt .Godlove Mbwanji alisema  mbali ya kutoa elimu kundi hilo pia wameweza kutoa kutoa elimu  kwa wafanyakazi wa hospitali.

Dkt. Mbwanji alisema kwamba wameona  ni muhimu kutoa elimu kwa kundi hilo kutokana na hali halisi ya mazingira ya watu wenye ulemavu wa kusikia ilivyo.

“Ni muda mwafaka kusaidia kundi hili ili lisiweze kuangamia na gonjwa hili hatari ,tumejitahidi kuwakusanya kwa pamoja na kuwapa elimu hii muhimu kwao ili waweze kujikinga”alisema  Mkurugenzi huyo.

Aidha Dkt. Mbwanji alisema kuwa mbali ya kutoa mafunzo hayo hospitali  imechukua tahadhari nyingine ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wodini kwa kuruhusu watu wachache kuingia wodini kuona wagonjwa.

Alisema kuwa kwa kuanzia walianza kutoa elimu kwa ndugu wa wagonjwa  katika kupunguza idadi ya ndugu ambao wanakuja kuona wagonjwa ambao wataingia ndugu wawili kila wakati  kwa kupeana nafasi  ya kuingia  kwa kadi maalum pamoja na kunawia  dawa ya vitakasa mikono.

Hata hivyo Dkt. Mbwanji alisema hivi  sasa kila mmoja amechukua tahadhari ya kupambana na ugonjwa huu kwa kunawa mikono pia kuweka vitakasa mikono maeneo ya ofisi na biashara yakiwemo masoko.