April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwazi na Uwajibikaji waleta tija Korogwe

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MRADI wa kukuza uwazi na uwajibikaji katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, umekuwa na matokeo chanya baada ya wananchi kuonesha kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwapelekea miradi ya maendeleo na kushiriki kuchangia nguvu zao (msalagambo).

Hayo yalisemwa jana (April. 2) na  Meneja Miradi wa Shirika la CETA lenye Makao Makuu yake mkoani  Dar es Salaam Goodluck Justin chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la HSF, wakati anatoa mrejesho wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mradi kwa mwaka 2019, kwa Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.

“Mradi umekuwa na matokeo chanya katika maeneo makubwa manne ikiwemo kuongezeka kwa uelewa, hamasa, mahudhurio, na ushiriki wa wananchi katika mikutano ya jamii na shughuli za maendeleo, kwani kuongezeka kwa uelewa wa viongozi wa vijiji na vitongoji katika kutekeleza wajibu na majukumu kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, kumeongeza ufanisi wa shughuli za kila siku za vijiji.

“Lakini pia, kuimarika kwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi hasa katika ngazi ya Kijiji na Kitongoji na kuongezeka kwa michango ya wananchi katika miradi ya maendeleo” alisema Justin.

Justin alisema katika Kijiji cha Kerenge- Makaburini Kata ya Kerenge, uongozi wa kijiji umeweza kufungua akaunti ya benki ya kijiji, kutenga eneo la kujenga Ofisi ya Serikali ya Kijiji, ambapo wananchi walijitolea nguvu kazi kusafisha eneo la ujenzi huo pamoja kuchangia vifaa vya ujenzi kama mawe, na kufanyika kwa zoezi la kutambua idadi ya kaya na nguvu kazi katika kijiji kwa ajili ya kuchangia maendeleo. Jumla ya Kaya 700 na Nguvu Kazi 1,000 ziliweza kubainika.

Katoka Kijiji cha Makangara, Kata ya Magoma, hamasa ya wananchi kushiriki mikutano ya kijiji imeongezeka, kwani kwa sasa ongezeka la mahudhurio kwenye mikutano ya kijiji ni kubwa. Na pia wananchi wa kijiji hicho wanajitolea katika ujenzi wa Zahanati ya Kijiji

Katika Kijiji cha Kijango, Kata ya Magoma, maudhurio ya wananchi katika mikutano ya kijiji imeongezeka kutoka 80 hadi 160 kwa sasa. Wananchi wamejitolea kusafisha eneo la kujenga Zahanati ya Kijiji. Pia wananchi wamejitolea vifaa vya ujenzi hasa mawe kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.Kwa sasa kuna mradi wa maji safi, nawananchi wameanza mchakato wa kuchangia sh. 1,000 kila mmoja kwa ajili ya kununua tenki la kuhifadhia maji. 

“Katika Kijiji cha Kerenge Kibaoni uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa mikutano ya Kijiji na Vitongoji umeongezeka. Pia kuongezeka kwa mahudhurio ya wananchi katika mikutano ya kijiji. Wananchi wanachangia fedha sh. 4,000 kwa kila kaya kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kerenge, na kuimarika kwa demokrasia katika mikutano mikuu ya kijiji, kwa sasa viongozi wanawasikiliza wananchi na wanawapa fursa ya kueleza kero zao” alisema Justin.

Justin alisema kila kaya imechangia sh. 8,500 kwa ajili ya kuongeza darasa katika Shule ya Msingi Kerenge- Kibaoni. Pia wananchi walishiriki katika kukarabati chumba cha darasa katika shule ya msingi baada ya kuezuliwa na upepo mkali

Vijiji vingine vilivyonufaika na mradi huo ni Songea, vingo, Kwagunda, Mnyuzi, Kwamzindawa, Gereza Mashariki, na huko kote wananchi wanatekeleza miradi mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la CETA Safari Minja alisema bado wataendelea kutoa elimu kwa vijiji vingine kwenye Wilaya ya Korogwe, kwani bado kuna changamoto nyingi kwenye vijiji ikiwemo viongozi wa vijiji kuuza ardhi kinyume cha utaratibu, huku baadhi ya wenyeviti wa vijiji wakihodhi mpaka madaraka ya viongozi wa kamati za vijiji.