March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari feki kizimbani kwa kifo cha mjamzito

Na Allan Ntana

WATU 3 wanaomiliki  maduka ya dawa mkoani Tabora wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora kwa makosa ya kusababisha kifo cha mwanamke mjamzito aitwaye Esta Chimika na mtoto aliyekuwa tumboni kwa kujifanya wahudumu wa afya na kumzalisha mwanamke huyo kisha kumsababisha kifo.

 Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora Jovita Kato wakili wa serikali mwandamizi Juma Masanja amesema katika shitaka la kwanza mnamo Machi 15, 2020 majira ya saa tisa mchana.

Alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Ezekiel Kazimoto Masanja,Victoria Boniface Makamba na Regina Florence Balaye wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa tabora na kusomewa mashitaka mawili ya mauaji.

Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walisababisha kifo cha Ester Chimika baada ya kujifanya wahudumu wa afya (waganga) na kumzalisha mwanamke huyo katika kijiji cha miswaki halmashauri ya wilaya ya Uyui, ambapo katika kosa la pili wanashitakiwa kwa kuharibu mtoto ambaye angezaliwa akiwa hai na makosa yote ni kinyume cha kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo na wamerudishwa mahabusu hadi tarehe 14/4/2020 kwa ajili ya kutajwa tena.