September 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waongezewa nguvu huduma za mama wajawazito Same

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira

HUDUMA za afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Same zinatarajiwa kuimarika baada ya Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania, kukabidhi vifaa vya kujifungulia kwa ajili ya akina mama wajawazito kupitia Kampeni yake ya Tumaini.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia, viti mwendo, mashuka, khanga, aproni na maternity kits ambavyo vinahitajika hasa wakati wa kujifungua.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo, amesema msaada huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni kutumia uwepo wake katika jamii kuleta mabadiliko yanayogusa maisha ya watanzania moja kwa moja.

“Kwetu Yas, tunapoendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano, tunaona ni muhimu pia kushirikiana na jamii tunazohudumia.

“Kupitia Kampeni ya Tumaini, tunataka mchango wetu uwafikie akina mama wajawazito moja kwa moja na kusaidia kuboresha huduma wanazopata wakati wa kujifungua,” amesema Kinabo.

Amesema, sehemu ya vifaa hivyo imetokana na michango ya wafanyakazi wa Yas kupitia Kampeni ya Tumaini, huku vingine vikichangiwa na Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) cha kampuni hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Same, Endutuja Mbwambo, ameishukuru Kampuni ya Mawasiliano ya Yas kwa msaada huo na kusema kuwa hospitali bado inauhitaji mkubwa wa vifaa hivyo kwani takribani wanawake 270-300 wanajifungua kila mwezi hospitalini hapo

Amesema, vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma za uzazi na kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wake.

Kampeni ya Tumaini inaendelea kufikia vituo mbalimbali vya afya nchini ikiwa na lengo la kusaidia huduma za afya ya mama na mtoto.