Na Mwandishi Wetu
TUME ya Ushindani ya Somalia imefanya ziara ya siku moja nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza uzoefu na mbinu zinazotumiwa na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) katika kusimamia ushindani wa kibiashara, kudhibiti bidhaa bandia na kulinda maslahi ya walaji.
Ziara hiyo imefanywa na Mkurugenzi wa Masuala ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na Kamishna wa Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki (EACA), Ahmed Warsame, pamoja na Mkurugenzi wa Biashara na Upatikanaji wa Masoko wa Wizara ya Biashara na Viwanda ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Abdihalim Osman.
Ujumbe huo ulikutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, pamoja na uongozi wa Tume, ambapo walijifunza namna FCC inavyotekeleza majukumu yake ya kukuza na kulinda ushindani, kulinda walaji na kudhibiti bidhaa bandia.
Akizungumza jana wakati wa ziara hiyo, uongozi wa ujumbe wa Somalia umepongeza utendaji wa FCC, ukieleza kuwa uzoefu wa Tanzania katika kusimamia ushindani na kulinda walaji ni muhimu kwa Somalia katika kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa soko na kujenga mazingira bora ya biashara.
Ujumbe huo umeeleza kuwa kujifunza kutoka FCC kutasaidia kuongeza uelewa na uwezo wa taasisi za Somalia katika kukabiliana na changamoto zinazohusu ushindani usio wa haki, bidhaa bandia na vite
ndo vinavyoweza kuwadhuru walaji.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na taasisi za Somalia na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi wa ushindani na ulinzi wa walaji.
Ziara hiyo imekuwa fursa kwa Somalia kujifunza uzoefu wa Tanzania katika ushindani wa kibiashara, udhibiti wa bidhaa bandia na ulinzi wa walaji, huku ikitarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kuchangia katika ujenzi wa masoko yenye ushindani wa haki na biashara endelevu.

More Stories
Waongezewa nguvu huduma za mama wajawazito Same
Wasusi watakiwa kutumia programu ya “Darling Hair” kujiimarisha
Madiwani Nkasi wataka mianya ya upotevu wa mapato izibwe