May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake watengwa maamuzi ya Familia


Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma


SERIKALI imeeleza kuwa wanawake wengi nchini bado hawana nafasi ya kutosha kushiriki katika maamuzi ya kijamii na kiuchumi, hali inayochangia kuendelea kwa pengo la kijinsia katika familia na jamii.


Hayo yamebainishwa kupitia matokeo ya Tafiti ya Uwezeshaji wa Wanawake na Lishe 2023/24 pamoja na Tafiti ya Jinsia na Mazingira 2025 zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwinu (NBS) na kuzinduliwa jijini Dodoma.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema wanawake wengi bado hawapati nafasi ya kutoa maamuzi muhimu licha ya mchango wao mkubwa katika maendeleo ya familia na uchumi wa jamii.


Amesema utafiti umeonesha kuwa ni asilimia tisa pekee ya wanawake wanaohisi wana uwezo wa kuzungumza na kusikilizwa katika jamii, jambo linaloonesha changamoto kubwa ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi.


Kwa mujibu wa matokeo hayo, wanawake wengi hushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na shughuli za kidini, lakini bado ushawishi wao katika maamuzi makubwa ya kifamilia na kijamii ni mdogo ukilinganishwa na wanaume.


Aidha, ni asilimia 26 tu ya wanawake wanaoamini wanapaswa kuwa na uhuru wa kuamua kuhusu shughuli zao za kiuchumi, huku wanaume wakitajwa kuendelea kuongoza katika maamuzi mengi ya matumizi ya fedha ndani ya familia.


Utafiti huo umeonesha kuwa wanaume wana nafasi kubwa zaidi katika kupanga matumizi ya fedha kwa asilimia 54.8, ikilinganishwa na asilimia 39.6 ya wanawake.


Dkt. Gwajima amesema hali hiyo inawanyima wanawake nguvu ya kufanya maamuzi kuhusu mapato wanayoyachangia wenyewe na kuathiri ustawi wa familia pamoja na maendeleo ya jamii kwa ujumla.


Katika upande wa lishe, amesema tafiti hizo zimebaini kuwa wanawake wenye uwezo wa kiuchumi wana nafasi kubwa ya kuboresha afya na lishe ya familia zao, hivyo kuonesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uwezeshaji wa wanawake.


Pia amesema wanawake ndio wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya vijijini ambako hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuni kutokana na ukame.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, karibu nusu ya kaya zilizopo katika maeneo yenye ukame zimeathirika na changamoto ya upungufu wa maji na chakula, hali inayotajwa kuhatarisha maisha na kipato cha wananchi.


Kutokana na matokeo hayo, Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu, mikopo na umiliki wa mali kwa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za maamuzi na kuchochea maendeleo jumuishi.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Anne Makinda amesema tafiti hizo zitasaidia Serikali na wadau mbalimbali kupanga sera na mikakati inayotegemea takwimu sahihi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi.