May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda :Serikali yawekeza katika Akili Unde kuandaa vijana

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua mahsusi za kuijengea Tanzania uwezo katika teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence – AI) ili kuhakikisha nchi inanufaika na mabadiliko ya teknolojia duniani badala ya kuathirika nayo.

Profesa Mkenda amesema hayo leo Mei 7,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo amesema,maendeleo ya haraka ya teknolojia ya akili unde duniani yamefungua fursa kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, elimu, ulinzi na usalama, lakini pia yanaweza kuleta changamoto endapo nchi haitakuwa na wataalamu wa kuimudu teknolojia hiyo.

“Akili unde inaweza kuboresha tiba na afya, kuongeza tija katika kilimo, kuimarisha elimu na kubadili namna nchi zinavyosimamia mifumo ya ulinzi na usalama. Hata hivyo, inaweza pia kuwa changamoto kubwa kama taifa halitakuwa tayari kuielewa na kuisimamia,” alisema Profesa Mkenda.

Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kubadili mfumo wa ajira duniani na kusababisha baadhi ya kazi kupotea kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali inatambua umuhimu wa kujenga uwezo wa taifa katika matumizi salama na yenye tija ya akili unde pamoja na teknolojia nyingine za kisasa ili maendeleo hayo yawe fursa kwa Watanzania.

Katika hatua ya kuimarisha uwezo huo, Serikali imeanzisha mpango maalumu wa ufadhili wa masomo unaojulikana kama Samia Scholarship Extended DS/AI+ unaolenga kuwapeleka vijana wa Kitanzania kusomea masuala ya akili unde na teknolojia zinazohusiana nayo katika vyuo vikuu vya nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, wanafunzi 50 wenye ufaulu wa juu zaidi katika tahasusi za sayansi zinazojumuisha hisabati katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2025 walichaguliwa kwa ushindani na uwazi kunufaika na mpango huo.

Amesema kabla ya kuondoka kwenda masomoni, wanafunzi hao walipelekwa katika kambi maalumu ya maandalizi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Arusha.

“Kati ya wanafunzi hao, 16 tayari wameanza masomo katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, huku wanafunzi 34 waliobaki wakitarajiwa kujiunga na vyuo vikuu nchini Ireland,” amesema.

Amefafanua kuwa kati ya wanafunzi hao wanaokwenda Ireland, wanafunzi 32 watajiunga na Chuo Kikuu cha Limerick huku wawili wakijiunga na Chuo Kikuu Kishiriki cha Dublin.

Profesa Mkenda amesema Serikali imefanikiwa kupata punguzo la asilimia 50 ya ada ya masomo kwa wanufaika wa mpango huo katika Chuo Kikuu cha Limerick kupitia makubaliano yaliyosainiwa Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema makubaliano hayo yanalenga kuongeza fursa kwa vijana wa Kitanzania kusoma fani za kisasa ikiwemo sayansi ya data, akili unde na sayansi shirikishi ili kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya teknolojia.

Kwa upande wa wanafunzi waliokwenda Chuo Kikuu cha Johannesburg, amesema wamefaidika na utaratibu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaowaruhusu kulipa ada nafuu ikilinganishwa na wanafunzi kutoka mataifa mengine ya nje ya ukanda huo.

Profesa Mkenda amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 inayolenga kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa hususan katika maeneo ya sayansi na teknolojia.

Ametoa wito kwa wadau wa elimu na maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia mfuko wa Samia Scholarship ili kuongeza idadi ya vijana wanaopata nafasi ya kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).