April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza wazindua ajenda kutetea haki zao nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dae

WANAOISHI na Magonjwa Yasiyoambukiza wameunda jukwaa lao na kuzindua ajenda ya utetezi wa haki zao za msingi katika kupata matibabu, kutunzwa kiafya, kushirikishwa katika uamuzi wa mambo yanayowahusu na kukomesha unyanyapaa.

Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Omary Ubuguyu alizindua ajenda hiyo jijini Dar es Salaam akiwahimiza washirikiane na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili.

“Tushirikiane kutafuta ufumbuzi. Si vyema tukabaki kulalalmika na kuainisha tu matatizo bali fikirieni pia namna tunavyoweza kushirikiana katika kufikia ufumbuzi wa matatizo,” alisema Dk Ubuguyu.

Kwa mujibu wa kitabu cha agenda waliyoizindua, magonjwa makuu yasiyoambukiza nchini ni moyo, mfumo wa hewa, kisukari, saratani, afya ya akili, sikoseli, figo, meno, magonjwa ya macho, masikio na majeraha.

Awali, Katibu wa jukwaa hilo, Norbert Silayo alisema: “Sisi tumeungana pamoja watu tunaoishi na magonjwa yasiyoambukiza ili kupaza sauti zetu na kuomba haki zetu juu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, matibabu stahiki na huduma ya kujimudu ambazo zinapatikana kwa bei nafuu na kwa wakati.”

Alisema magonjwa yasiyoambukiza yanatuathiri kimwili, kiakili, kihisia, kijamii na kiuchumi na maelfu ya Watanzania wanapoteza maisha yao kwa sababu ya magonjwa haya kila mwaka.

Akielezea madhila wanayopata, Silayo alisema wanapata changamoto ya gharama kubwa za matibabu na dawa, kucheleweshwa kwa utambuzi, ukosefu wa huduma za ushauri na gharama kubwa za kusafiri kwenda kwenye vituo vya afya.

Isitoshe, akasema wanakabiliana na unyanyapaa katika maeneo mbalimbali kama vile kazini, shuleni na katika jamii.

Mmoja wa wanaougua kisukari, Jackob Mwambi alisema: “Wito kwa serikali, viongozi na jamii ni kutambua uzoefu wetu wa kuishi na magonjwa yasiyoambukiza kama kichocheo muhimu cha kufanya mabadiliko ya sera na afua kwa wananchi.

Washiriki wa uzinduzi wa agenda ya utetezi kwa wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza wakionesha furaha mara baada ya uzinduzi.

“Ili kubadilisha maisha yetu, tunapendekeza kuwa sehemu ya hatua za maamuzi na mawasiliano katika ngazi zote ikiwemo jamii na kuhakikisha kuwa maoni na sauti zetu zinasikika.”

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasioyoambukiza (TANCDA) ndilo lilisimamia kuundwa kwa jukwa hili na kusimamia harakati zao hadi kukamilisha utengenezaji wa ajenda hiyo.

Meneja miradi wa TANCDA, Happy nchimbi alisema ajenda ya utetezi ya watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza nchini Tanzania ilitengenezwa kufuatia mpango anzilishi wa “Maoni Yetu, Sauti Zetu” wenye dhumuni la kuhamasisha uhusika wa kina wa watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza katika kupambana na magonjwa hayo.

Amesema katika mpango huo TANCDA iliweka pamoja zaidi ya watu 200 wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza, wakiwemo wenza au ndugu wanaowatunza ambao walibainisha mahitaji yao, changamoto, na vipaumbele vyao kuhusiana na kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Mmoja wa wanaharakati hao, Neema Mohamedi alisema: “Tunaamini kwa dhati kwamba hatua kubwa ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na kupunguza
udhaifu ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu na haki za kijamii za raia wote wa Tanzania zinalindwa.”

Naye, Bora Hilary akasema wanataka wachukuliwe kwa heshima na utu, kushirikishwa katika kutengeneza na kusimamia sheria, sera, kanuni na miongozo inayolinda haki zao katika ngazi zote.