April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Je unajua hasira hasara? Soma jinsi unavyoweza kudhibiti hasira zako

Na Ulumbi Enock

Ulumbi Enock ni Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

TUNAPOPATA hisia ya hasira huwa inaambatana na mabadiliko kwenye kiwango cha kisaikolojia na kibaolojia.

Kama vile kiwango cha moyo wetu au shinikizo la damu huongezeka, pamoja na kiwango cha usiri wa homoni fulani,kama adrenaline na noradrenaline.

Kwa mtazamo wa saikolojia, hasira inaweza kujidhihirisha na viwango anuwai vya ukali, kulingana na sababu zinazosababisha.

Kwa hivyo, hasira inaweza kuonyeshwa kwa onyo nyepesi la maneno au kwa ghadhabu isiyo ya kawaida ambayo inaweza hata kuwa hatari ikiwa mtu anayeugua hajui jinsi ya kuishughulikia.

Acid ni kemikali ambayo ni hatari sana,kemikali hii inapowekwa katika chombo huathiri zaidi chombo hicho kuliko vitu vingine vyote vilivyopo jirani na chombo hicho.

Vivyo hivyo ndivyo mtu anapokuwa na hasira,kwani hasira ni hali ambayo humuathiri zaidi aliyenayo kuliko mtu mwingine zaidi,kwani maumivu ya hasira huyapata yle aliyenayo zaidi kuliko aliyechanzo cha hasira hiyo.

Kila kiumbe aliye hai hupatwa na hasira,yaani wanyama,ndege na hata wadudu wote hupatwa na hasira.Hivyo hasira ni hali isiyoepukika katika hali ya kawaida.

Mwanasaikolojia T.W Smith yeye anasema kuwa,hasira ni muhemko usio epukika,unaotokana na hisia hasi juu kitu,jambo au hali fulani. Muhemko huu hutofatiana kutoka katika hali ya kawaida hadi katika hali inaweza kusababisha madhara kwa mtu mmoja na hata kwa watu wengine.

SABABU KADHAA ZINAZOSABABISHA HASIRA

Kuumizwa kwa njia yoyote ile bila sababu yoyote ile,hii hutokea zaidi katika mahusiano hasa ya kimapenzi,kulazimishwa kufanya jambo au kitu usichokipenda,kutokutendewa haki unayostahili bila kujalisha ni kweli ama si kweli.

Vitisho na mawazo ambayo hupendezewi nayo katika maisha.Msongo wa mawazo pia ni chanzo kikubwa cha hasira,kwani mtu anapopata msongo wa mawazo maana yake anakua na mkusanyiko wa mambo mengi sana kichwani ambayo yamekosa suluhisho la kuyapunguza.

Hivyo anakuwa na uwezo wa kufanya chochote atakachoamua,hivyo hasira zake zipo karibu zaidi.Kukataliwa katika jambo au mambo ambayo huamini kuwa na thamani katika maisha yake ya kila siku.

Pamoja na sababu nyingine nyingi ambazo hutofautiana kati ya mtu na mtu,na huwa na hisia tofauti,huweza pia kupelekea mtu kupatwa na hasira.

Kumbuka:Kitu kinachoweza kukufanya wewe kupatwa na hasira za mara kwa mara,kinaweza kumfanya mtu mwingine kuwa na furaha au kuwa katika hali ya kawaida.

Hii yote hutokana na tafsiri juu ya jambo fulani ambapo tafsiri hiyo hupelekea kupatwa na hisia tofauti na uliyoitegemea katika jambo lile,na mwisho wake hupelekea kupatwa na hasira.Na hali huweza kupelekea ugumu katika kuielewa na kuizia hasira.

NINI ATHARI ZA HASIRA

Hasira inaweza kuzuilika,lakini pia kuna wakati hasira hushindwa kuzuilika na hatimaye mtu hukutana na changamoto mbalimbali na katika mazingira tofauti.

Kushindwa kupata suluhisho la matatizo mbalimbali unayokutana, Kushindwa kufanya maamuzi sahihi pale unapokutana na hali inayohitaji maamuzi.Kushindwa kujenga na kuimarisha mahusiano yaliyo imara na bora zaidi,haijalishi ni mahusiano ya aina gani.

Kupoteza uaminifu kwa watu wako wa karibu,na hii ni kutokana na jinsi unavyochukulia na kutafsiri mambo.

Huathiri zaidi utendaji na uwajibikaji katika majukumu ya kila siku kama vile biashara,masomo na hata shughuli za kiofisi.
Lakini pia mtu mwenye hasira za mara kwa mara huweza kuathiriwa kiafya na kujikuta amedhoofika sana.

Kuna utafiti uliofanywa na wasomi wa saikolojia huonyesha kuwa,mtu aliye na hasira za mara kwa mara huweza kupatwa na matatizo mengine kama vile;ugonjwa wa moyo(Cardinal heart disease),matatizo ya moyo.

NAMNA YA KUDHIBITI HASIRA

Unaweza kuzuia hasira yako pale unapoweza kuitambua mapema kabla haijawa na madhara kwako na kwa wengine pia.Hizi ni baadhi tu ya njia utakazoweza kutumia kuweza kuzuia hasira yako pindi utakapotambua kuwa imekaribia kuwa na madhara:

Tambua na kubali kuwa una tatizo na hapo anza kupanga jinsi ya kukabiliana na hilo tatizo.Tambua na uelewe kwa umakini na utulivu wa hali ya juu chanzo au vyanzo vya hasira yako kwa mtazamo chanya.

Shirikisha watu wako wa karibu na unaowaamini zaidi juu ya tatizo ulilo nalo,famili na rafiki zako wa karibu ndio watu wa muhimu zaidi.

Zuia mzunguko wakati wa hasira pale utakapoanza kuhisi hasira hasa kwa kutumia mbinu tofauti(Relaxation techniques) kama kuvuta hewa ndani kwa muda na kuitoa taratiiibu.

Chukulia tatizo linalokupa hasira kama ni la mwenzako na uhisi kama ni yeye,ungelichukuliaje(Empathy).Kumbuka kila mtu hukosea,na kupitia kukosea tunajifunza.

Weka na tengeneza furaha katika maisha yako na uchukulie changamoto kwako kama ni ushindi.Hapo utakua umeshinda kila kitu.Jifunze kucheka na kufurahi kila siku.

Jifunze kuwa msikivu na muelewa kwa kila kitu,kwani kutofautiana katika mawasilia ni chanzo pia cha hasira.Siku zote kuwa na kiasi kwa kila unachokifanya,heshimu unachokipenda na uheshimu pia uhitaji wa mwenzio.

Jifunze kuishi kwa muda na kufanya maisha yako kama yapo katika siku za mwisho.Kumbuka maishani mafupi sana,unapotumia muda mwingi kuwa na hasira unapunguza kwa kasi kubwa sana hizo siku zko chache zilizobaki.

SAMEHE NA SAHAU

Kumbuka: Anza leo kupatana na kila umwonaye hukusababishia hasira,najua ni ngumu sana kwa mazingira ya kawaida.Lakini ukiamua kujishusha na kufikiria kuwa bado una mambo mengi ya kufanya na hayajakamilika,huwezi kuziruhusu hisia zako kuwaza vibaya na hatimaye kukupeleka usipopataka.Na hapo utakua umepiga hatua kubwa sana katika maisha.

KUHUSU MWANDISHI

Ulumbi Enock ni Mwanasaikolojia kijana kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni mwanachama wa jamii ya wanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Dar es Salaam Psychology Association-UDPSA), jumuiya ambayo inahusika na ushauri wa kisaikolojia katika makundi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) kuhamasisha kujitambua na afya ya akili katika jamii.

Pia ni mjumbe wa Taasisi ya FIKRA ZETU, taasisi ambayo inahusika na utoaji elimu na jinsi ya kupambana na changamoto za kila siku maishani.