March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa dengu na choroko waiomba serikali idhibiti walanguzi vijijini

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga

Baadhi ya wakulima wa mazao ya dengu na choroko katika kijiji cha Manih’gana wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi katika uzinduzi wa msimu wa uuzaji wa dengu uliofanyika katika kijiji cha Manih’gana wilayani Shinyanga (Picha na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga)

SERIKALI mkoani Shinyanga imeombwa iendelee kuwachukulia hatua kali za kisheria walanguzi wanaonunua mazao ya dengu na choroko kutoka kwa wakulima kwa njia ya kuwalangua na badala yake iwahimize wakulima kuuza mazao yao kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani.

Ombi hilo limetolewa na wakulima wa Kijiji cha Manih’gana wilayani Shinyanga wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa uuzaji wa zao la dengu kwa mwaka 2021/2022 ambao umefanyika kwenye Chama cha Msingi cha Ikumbo Amcos katika kijiji cha Manih’gana kilichopo Kata ya Solwa.

Wakulima hao wamesema pamoja na Serikali kuhimiza suala la uuzaji wa mazao ya jamii ya kunde kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani, lakini bado wapo wanunuzi binafsi wanaopita vijijini wakiwarubuni wakulima na kununua mazao yao kwa bei ya chini.

Wamesema kibaya zaidi baadhi ya walanguzi hao wamekuwa wakipotosha ukweli juu ya dhamira nzuri ya Serikali ya kutaka wakulima kuuza mazao kwa mfumo huo kwa madai ya kwamba malipo yake yanachelewa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Solwa, Awadhi Mbarak amesema ili kuwezesha mfumo wa stakabadhi ghalani ufanikiwe na uwe na matokeo yenye tija ni juu ya Serikali kuusimamia kwa ukaribu ikiwemo kuwachukulia hatua za kisheria walanguzi wanaokwenda vijijini kukusanya mazao kwa njia ya vificho.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Shinyanga (SHIRECU), Kwiyolecha Nkilijiwa (wa pili kutoka kushoto) akimtambulisha kwa baadhi ya viongozi wa Kata ya Solwa wilayani Shinyanga mgeni rasmi katika uzinduzi wa msimu wa uuzaji wa zao dengu, Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude (Mwenye suti ya bluu). (Picha na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga)

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa yote yaliyozungumzwa hapa ni mambo ya msingi, wewe ndiye tunayekutegemea katika hili, kwakweli bila Serikali kutusimamia suala hili halitawezekana, mkono wa Serikali ukiwepo yote yatawezekana,” ameeleza Awadhi.

Diwani huyo pia alitoa wito kwa wakulima wote kuhakikisha hawakubali kuuza mazao yao kwa walanguzi na badala yake wapeleke mazao yao kwenye vyama vyao vya msingi ili yauzwe kwa njia ya mnada na kuwawezesha kupata bei nzuri tofauti na inayotolewa na walanguzi.

Mmoja wa wakulima wa zao la dengu aliyejitambulisha kwa jina la Pombe wa Pombe mkazi wa Kijiji cha Manih’gana amesema ili kuwa na mafanikio katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani ni lazima Serikali iwasimamie kwa karibu zaidi.

“Kwa kweli hawa walanguzi wamekuwa watitupunja sana, maana pamoja na wengine kudai wanatoa bei nzuri, lakini vifaa vyao wanavyopimia mazao yetu vyote vimechezewa, vinachukua mazao mengi kwa lengo la kuwawezesha wao kupata faida kubwa,”

“Sasa tuiombe Serikali iwasake na kuwakamata na hata ikibidi itoe ruhusa kwa walinzi wa jadi (Sungusungu) tulionao huku vijijini wawe wanawakamata pale wanapowaona wakipita vijijini kukusanya mazao, wanatupunja sana, nguvu zetu zinapotea bure,” ameeleza Pombe wa Pombe.

Katika risala yao kwa mgeni rasmi, Kaimu Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika Mkoani Shinyanga (SHIRECU), Edson Ngulimi amesematangu Serikali ilipoagiza kuanza kutumika kwa mfumo wa uuzaji wa mazao ya jamii ya mkunde kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani wakulima wameanza kuona faida yake.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude akiwahutubia wakulima wa mazao ya dengu na choroko katika kijiji cha Manih’gana wilayani Shinyanga wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa uuzaji dengu ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati. (Picha na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga)

Ngulimi amesemakatika msimu wa mwaka jana wakulima wa choroko mkoani Shinyanga walijipatia zaidi ya shilingi bilioni nane baada ya kuuza kwenye mnada choroko zenye uzito wa kilogramu 5,566,804 kwa bei ya juu ya shilingi 1,620 kwa kilo moja huku Halmashauri zikipata ushuru wa shilingi milioni 194.866.

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoani Shinyanga, Hilda Boniface amesemachangamoto ya uwepo wa walanguzi kwenye ununuzi wa mazao ya choroko na dengu imechangia kwa kiasi kikubwa kusuasua kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani ambapo hata amesemakutokana na elimu ambayo imeendelea kutolewa kwa wakulima wengi wao wameanza kuona manufaa yake.

“Pamoja na changamoto zilizopo, bado wana Ushirika wengi wameendelea kupiga simu kuulizia juu ya utekelezaji wa mfumo huu, hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM),”

“Mheshimiwa mgeni rasmi, katika msimu uliopita wakulima wetu wamefanikiwa kuuza zaidi ya kilo milioni sita za choroko kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani, na leo hii tunategemea kupata maelezo kutoka kwako ya namna gani tutaimarisha huu mfumo,” ameeleza Boniface.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati katika hotuba yake ambayo ilisomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude amesema kuanzia sasa Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika kuchezea mfumo wa Stakabadhi ghalani.

“Naomba niwaambie umma wa wana Shinyanga, kwamba sintawachekea wale wote ambao ama kwa makusudi au kwa maslahi yao binafsi watakaobainika kuhujumu mfumo huu wa Stakabadhi ghalani ndani ya mkoa wetu wa Shinyanga na kukwamisha dhamira njema ya Serikali kwa wakulima wake,”

“Watu wa aina hii mara zote wamekuwa hawana nia njema kwa wakulima pamoja na Serikali iliyoleta mfumo huu wenye lengo la kumnufaisha mkulima, ninaagiza kwamba mazao yote ya choroko na dengu yaendelee kuuzwa kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani kama ilivyoelekezwa kwenye muongozo uliotolewa na Tume ya Ushirika,” ameeleza Mkude.

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga, Hilda Boniface akitoa taarifa kwa mgeni rasmi juu ya utekelezaji wa utaratibu wa uuzaji mazao ya jamii ya mkunde kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani kwenye uzinduzi wa msimu wa uuzaji dengu uliofanyika katika kijiji cha Manih’gana wilayani Shinyanga. (Picha na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga)