Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
WAUMINI wa Kiislamu mkoani Mwanza wameaswa kudumisha amani, upendo na mshikamano katika jamii pamoja na kuendeleza matendo mema walioyafanya katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Miongoni mwa matendo hayo ni pamoja na kulipa zaka na kuyajali makundi yenye uhitaji, hususani yatima, ili kuimarisha ustawi wa kijamii na mshikamano wa kitaifa.

Wito huo ulitolewa Machi 21,2026 na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, baada ya sala ya Idd El Fitri iliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Nyamagana,ambapo amesisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa dini ya Kiislamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Amesema bila amani, ibada haziwezi kufanyika ipasavyo na hata juhudi za maendeleo hushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa sababu ya vurugu.Aliwasihi waislamu kuilinda na kuihubiri amani katika maisha yao ya kila siku na kuheshimu viongozi wa dini na serikali.
“Amani ya kule tunakokwenda kuhiji imeharibika, twende kuiombea dunia amani iwe sehemu salama ya kuishi.Tuiombee Tanzania izidi kuwa kisiwa cha amani, tumwombee Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, maana yapo baadhi ya mataifa yanawaondoa madarakani viongozi wao,”amesema Sheikh Kabeke.
Pia amewataka waumini hao,kushikamana na kuepuka migawanyiko inayotokana na ukabila, ukanda, taasisi au mitazamo tofauti, akisisitiza umuhimu wa kujenga umoja wa kitaifa.
Aidha amesema,ni vyema kwa waislamu kuishi kwa amani na watu wa imani za dini nyingine, akieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kinachopaswa kulindwa kwa vitendo.
Huku akuwahimiza waumini hao kutekeleza wajibu wa kutoa zaka, akibainisha kuwa kama kuna jambo litakalosababisha kuchomwa moto ni zaka iliyo nguzo muhimu ya Uislamu.
“Utoaji zaka unapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa,na kushindwa kutoa zaka kwa wenye uwezo ni kinyume cha mafundisho ya dini,”amesema Sheikh Kabeke.
Sheikh Kabeke akizungumzia vijana, ameonya kuhusu mmomonyoko wa maadili,ambapo amesema baadhi yao wanajihusisha na vitendo visivyo na tija mitandaoni na kuiga mambo ya ovyo, badala ya kufanya kazi halali huku wakichagua aina ya kazi.

Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, zitakazowawezesha kusaidia dini yao, kujenga uchumi wao na taifa, huku Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa, akiwataka waumini kusherehekea Idd El Fitri kwa amani, upendo, mshikamano na kuzingatia utu.


More Stories
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni