April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya bil.2.9 kulipa fidia waliopitiwa na mradi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya

WANANCHI waliopitiwa na utekelezaji wa mradi wa maji wa Mto Kiwira wametakiwa kuwa na utulivu wakati taratibu za ulipaji fidia zikiendelea kufuatwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya, Mhandisi Barnabas Konga, amesema Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi walioathiriwa na mradi huo.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayestahili fidia anapata haki yake kwa wakati ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.

Mhandisi Konga amesema pamoja na mradi huo kufikia takribani asilimia 49 ya utekelezaji, hatua za fidia zinaendelea sambamba na ujenzi, huku rasilimali za kutosha zikitengwa kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi na usawa.

“Kukamilika kwa mradi huu kutaboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Mbeya na maeneo jirani, na kupunguza uhaba wa maji kwa wananchi,” amesema Mhandisi Konga.

Aidha, amewahimiza wananchi kushirikiana na mamlaka husika ikiwemo RUWASA ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, akisisitiza kuwa manufaa yake yatakuwa makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi, amesema kazi ya ujenzi wa tenki la maji la Forest inaendelea, ambapo hatua iliyopo ni usukaji wa nondo, huku mkandarasi akiwa tayari ameagiza saruji kutoka kiwanda cha Dangote. Amesema baada ya saruji kufika, kazi ya umwagaji zege la juu itaanza.

“Hii kazi ya kumwaga zege itafanyika kwa siku mbili hadi tatu mfululizo kwa kutumia mashine maalum ya kusukuma zege itakayofanya kazi muda wote,” amesema.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Joseph Dalabi, amesema utekelezaji unaendelea kwa kasi ndani ya muda uliopangwa, ambapo kwa sasa wanaandaa mazingira ya umwagaji zege kwa kutumia mitambo ya kisasa kwa saa 24 ndani ya siku tatu.