April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JAI yagawa chakula kwa Wagonjwa Muhimbili na Mloganzila

Na Penina Malundo,Timesmajira

Taasisi ya Jumuiya ya Tabia za Kiislamu (JAI) imetoa msaada wa chakula chenye uzito wa zaidi ya kilo 500 kwa wagonjwa na ndugu wanaowahudumia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na kituo chake cha Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kusherekea sikukuu ya Eid Alfitr na kuwafariji wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JAI, Ridhiwani Mpanju amesema kuwa katika kusherehekea Eid al‑Fitr mwaka huu, jumuiya hiyo ilipanga kuandaa chakula maalum na kula pamoja na wagonjwa hao ili kuwapa faraja na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na jamii.

Amesema lengo la msaada huo ni kuonesha mshikamano na kuwapa faraja wagonjwa pamoja na familia zao katika kipindi wanachopitia changamoto za kiafya.

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2008 kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2014, ikiwa na dhamira ya kuwahudumia wagonjwa na kuwapa faraja katika kipindi wanachopitia changamoto za kiafya.

Amesema kupitia makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyopo Magomeni, wamekuwa wakitekeleza shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwapatia wagonjwa uji wa asubuhi na chakula cha kufuturu wakati wa mwezi wa Ramadhani, pamoja na kusaidia kulipia bili za wagonjwa waliokwama hospitalini.

Aidha amesema JAI kuwaitaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za afya na jamii kwa ujumla ili kusaidia makundi yenye uhitaji na kuimarisha mshikamano wa kijamii .

Baadhi ya wagonjwa na ndugu waliopokea msaada huo walishukuru taasisi hiyo kwa kuwajali na kuwasaidia katika kipindi kigumu, wakisema chakula hicho kitawapunguzia mzigo wa gharama za kila siku wakati wa matibabu.